Upatikanaji wa maji vijijini Shinyanga wafikia asilimia 70

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 11:57 AM Sep 19 2025
Meneja wa RUWASA mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Julieth Payovela akitoa maelekezo ya hali ya upatikanaji wa maji vijijini katika bodi ya maji ya Ruwasa ilivyofika mkoani hapa.
Picha: Shaban Njia
Meneja wa RUWASA mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Julieth Payovela akitoa maelekezo ya hali ya upatikanaji wa maji vijijini katika bodi ya maji ya Ruwasa ilivyofika mkoani hapa.

Mkoa wa Shinyanga umeendelea kupiga hatua kubwa katika sekta ya maji baada ya kufanikisha ongezeko la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kufikia asilimia 70, hatua inayotajwa kuchangia kupungua kwa magonjwa ya mlipuko.

Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Julieth Payovela, ameeleza hayo leo mbele ya Mwenyekiti wa Bodi ya RUWASA, Mhandisi Lucy Koya, aliyekuwa ameambatana na wajumbe wake wakati wa kikao cha tathmini ya miradi ya maji kilichofanyika kata ya Bugarama, Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama.

Amesema kwa sasa mkoa huo unazalisha lita milioni 125.446 za maji kwa siku, ambapo vijijini zinapatikana lita milioni 42.7 zinazohudumia wananchi milioni 1.067 sawa na asilimia 70 kupitia vituo 9,631 vya kuchotea maji.

“Upatikanaji wa maji katika Halmashauri ya Kishapu ni asilimia 62.5, Wilaya ya Shinyanga asilimia 79.3, Ushetu asilimia 63.6 na Msalala asilimia 74. Kwa ujumla tumefikia wastani wa asilimia 70, na tumesalia na asilimia 15 pekee kufikia lengo la asilimia 85,” alisema Payovela.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA, Wolta Kirita, alisema shirika hilo litaendelea kutekeleza miradi ya maji vijijini kulingana na upatikanaji wa fedha, na kufikia mwezi Desemba mwaka huu kiwango cha upatikanaji vijijini kitafika asilimia 85.

Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya RUWASA, Mhandisi Lucy Koya, alimpongeza Meneja wa mkoa kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maji na kufanikisha kufikia asilimia 70 ya upatikanaji vijijini. Alisisitiza kuongezwa kasi ya utekelezaji wa miradi 20 inayoendelea ili kufanikisha malengo ya serikali ya kumtua mama ndoo kichwani.