Watanzania washauriwa kuilinda amani kama msingi wa maendeleo

By Ibrahim Joseph , Nipashe
Published at 07:55 PM Sep 18 2025
Ofisa Habari wa Umoja wa Mataifa (UN) Tanzania, Nafisa Didi
Picha: Ibrahim Joseph
Ofisa Habari wa Umoja wa Mataifa (UN) Tanzania, Nafisa Didi

Watanzania wameshauriwa kuendelea kuilinda amani iliyopo nchini bila kuchoka, kwa kuwa ndiyo msingi wa maendeleo endelevu ya Taifa. Kauli hiyo imetolewa na Ofisa Habari wa Umoja wa Mataifa (UN) Tanzania, Nafisa Didi, leo Septemba 18, 2025, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya siku ya amani.

Didi amesema licha ya uwepo wa amani nchini, bado kuna haja ya Watanzania kuendelea kuilinda, kwani bila amani hakuna maendeleo.

“Amani ndiyo kila kitu katika taifa lolote lile; hivyo kila mtu ana wajibu wa kuhakikisha anailinda hiyo amani ili iendelee kuwa nguzo muhimu katika taifa letu,” amesema.

Maadhimisho ya siku hiyo kitaifa yatafanyika Septemba 19, 2025, katika Mkoa wa Dodoma, licha ya siku ya kimataifa ya amani kuangukia Septemba 21, ambayo mwaka huu inafellishwa Jumapili. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Chukua Hatua Sasa, Ulinda Amani.”

Didi pia amesema kuwa wadau wamefanya jitihada za kutoa elimu kwa vijana kuhusu umuhimu wa amani, ambapo vijana 1,500 wamepatiwa mafunzo katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, na Dodoma.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Global Peace Foundation Tanzania, Hussein Sengu, ameweka mkazo juu ya umuhimu wa vyombo vya habari kuendelea kuhamasisha amani nchini. Alisisitiza kwamba vyombo vya habari vinapaswa kuweka ajenda maalumu ya kuelimisha wananchi kuhusu kulinda amani.

Sengu ameongeza kuwa hali ya amani ni muhimu, akitaja mfano wa eneo la Israel na Gaza, ambapo zaidi ya waandishi 200 wamepoteza maisha wakiwa katika kutekeleza wajibu wao wa kimaandishi.

“Tunapaswa kujifunza kutoka katika maeneo mengine duniani na kuthamini amani yetu hapa Tanzania,” amesema Sengu.