Wafugaji wa samaki wa vizimba Mwanza wapata suhulu gharama ya chakula

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:15 PM Sep 20 2025
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Happness Nditi
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Happness Nditi

Wadau wa sekta ya kilimo na uvuvi mkoani Mwanza wamekutana kwa kikao kazi kujadili changamoto kubwa inayowakabili wafugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ikiwemo tatizo la upatikanaji wa chakula cha samaki kwa gharama nafuu na zenye ubora.

Kikao hicho kimeandaliwa na Kampuni ya DEHA FISHFEED kwa lengo la kujadili na kuweka mikakati ya pamoja ya kutafuta suluhu ya changamoto zinazokwamisha vijana wengi waliopania kujiendeleza kupitia sekta ya ufugaji wa samaki.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Happness Nditi, alisema licha ya sekta ya ufugaji wa samaki kuonyesha mafanikio makubwa katika ukanda wa ziwa victoria, wafugaji wamekuwa wakikumbana na mzigo wa gharama kubwa kutokana na kulazimika kuagiza chakula nje ya nchi.

‘’Wafugaji wengi hawapati faida wanayostahili kwa sababu gharama za chakula ni kubwa mno. deha fishfeed imejipanga kuzalisha na kusambaza chakula chenye ubora na bei nafuu ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje na kuongeza tija kwa wafugaji,” alisema happness.

Wafugaji walioshiriki kikao hicho waliiomba serikali kurahisisha masharti na kutoa nafasi kwa wawekezaji kuanzisha viwanda vya ndani vya kuzalisha na kusambaza chakula cha samaki.

Beatrice Makoko, mmoja wa wafugaji wa vizimba, alisema gharama kubwa za chakula zimekuwa kikwazo kwa vijana wengi walioamua kujiajiri kupitia sekta hiyo.

‘’Tunajitahidi, lakini gharama za chakula zimetufanya wengine washindwe kuendelea. kama viwanda vya ndani vitapanua uzalishaji, tutapata nafuu kubwa na kuongeza uzalishaji,” alisema Beatrice



Wafugaji hao wameongeza kuwa uwepo wa viwanda vya ndani utawapunguzia gharama na kuwaongezea kipato na kusaidia kuzalisha a

jira mpya kwa vijana.

kwa upande wake, Elinsa Massawe, afisa mfawidhi wa idara ya ukuzaji viumbe maji kanda ya ziwa victoria, alisema serikali imeweka mkakati wa kutoa elimu na mafunzo kwa wafugaji ili kuhakikisha ufugaji wa vizimba unakuwa endelevu na kuchangia katika mapambano dhidi ya uvuvi haramu.

Naye Peter Masumbuko, mkufunzi mwandamizi kutoka chuo cha uvuvi (FETA) kanda ya Mwanza, alibainisha kuwa uwekezaji katika sekta ya chakula cha samaki si tu utapunguza gharama, bali pia utaongeza ubunifu na utafiti wa kitaalamu kuhusu aina bora ya lishe kwa samaki wa vizimba.

Wadau walikubaliana kuwa uwekezaji katika viwanda vya chakula cha samaki utasaidia kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi, kuongeza ajira kwa vijana na kuboresha kipato cha wafugaji.

Mkutano huo umeibua matumaini mapya kwa wafugaji wa samaki mkoani Mwanza, huku matarajio yakiwa kwamba serikali na sekta binafsi zitaungana kuwekeza katika miundombinu na teknolojia za kuzalisha chakula cha samaki nchini.