Katibu Mkuu wa CCM ampongeza Samia, Mwinyi kwa mchango wa maendeleo

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 07:46 PM Sep 18 2025
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Asha-Rose Migiro.
CCM
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Asha-Rose Migiro.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Asha-Rose Migiro, amemsifu Rais na mgombea urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kulinda na kudumisha Muungano, kuimarisha mshikamano wa kitaifa, na kuendeleza diplomasia iliyoweka Tanzania kimataifa.

Balozi Migiro alibainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na juhudi za Dk. Samia katika filamu ya Royal Tour, sera za kuvutia uwekezaji, ongezeko la watalii, utekelezaji wa miradi ya kimataifa ya miundombinu, na kuimarisha msingi wa uchumi shindani unaojikita kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kwa upande wa mgombea urais Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, Katibu Mkuu Migiro amempongeza kwa mageuzi makubwa ya kimaendeleo yaliyotekelezwa visiwani humo, hususan katika ujenzi wa miundombinu, huduma za jamii, na kuimarisha uwajibikaji wa taasisi.

“Sera zake za utalii na uchumi wa buluu zimeiweka Zanzibar kwenye ramani ya dunia kama kitovu cha uchumi wa kisasa, sambamba na kukuza ustawi wa wananchi,” amesema Migiro.

Akizungumza leo, Septemba 18, 2025, katika mkutano wa kampeni za CCM uliofanyika Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Balozi Migiro pia aliwatambulisha wananchi na kuwanadi wagombea hao, akieleza sifa zao na dhamira ya kuendelea kulitafsiri taifa kwa maendeleo endelevu.

Balozi Migiro amewahimiza wananchi wa Kaskazini Unguja na Watanzania wote kuendelea kuunga mkono wagombea wa CCM kwa kuwapigia kura ya “ndiyo,” ili kufanikisha utekelezaji wa ndoto za Dira 2050 kuwa uhalisia wa maisha ya kila Mtanzania.