Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mary Maganga, amelipongeza Baraza la Ushauri la Taifa kwa Watu wenye Ulemavu kwa mchango mkubwa walioutoa katika kuimarisha haki na ustawi wa kundi hilo nchini.
Amesema juhudi hizo zimekuwa chachu ya mafanikio katika kuendeleza ajenda ya usawa, ushirikishwaji na ulinzi wa haki za watu wenye ulemavu, hatua inayochangia kuimarisha maendeleo jumuishi ya kijamii na kiuchumi.
Maganga alitoa pongezi hizo leo, Septemba 18, 2025 jijini Dodoma, wakati wa kuhitimisha shughuli za utekelezaji wa baraza hilo kwa kipindi cha miaka mitatu (2022–2025).
Akieleza mafanikio yaliyopatikana kupitia baraza hilo, Maganga alitaja kukamilika kwa Mwongozo wa Uratibu wa Vyama vya Watu wenye Ulemavu (2025), Mkakati wa Taifa wa Teknolojia Saidizi (2024–2027), Mpango wa Taifa wa Haki na Ustawi wa Watu wenye Ualbino, Mwongozo wa Mfuko wa Taifa wa Watu wenye Ulemavu pamoja na Mwongozo wa Taifa wa Viwango vya Ufikivu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Dk. Lukas Kija, aliipongeza Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kutoa ruzuku kwa vyama vya watu wenye ulemavu, kusambaza vifaa saidizi na kuzindua mfumo wa kanzi data ya watu wenye ulemavu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED