Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi, Mohamed Hassan Moyo, ameonyesha hasira kali baada ya kubaini kuwa ujenzi wa Kituo cha Afya Nammanga kilichopo Kata ya Ruponda unaendelea bila kuzingatia makadirio ya mradi (BOQ).
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo, DC Moyo alisema serikali haiwezi kuvumilia wataalamu wanaokiuka taratibu na kujenga miradi ya umma chini ya kiwango.
“Leo hii jamvi linafunikwa bila utaratibu; nondo za mita nane zinatumika badala ya nondo za mita 12, na mbao zilizopangwa kujenga jengo moja zinatumika kujenga majengo mawili. Haya hayapo kwenye BOQ,” alisema kwa kusisitiza.
Kutokana na ukiukwaji huo, DC Moyo aliagiza TAKUKURU kuwakamata wahandisi wote wanaohusika na kuwapeleka mahakamani ili kujibu tuhuma za matumizi mabaya ya fedha na ujenzi usiozingatia viwango.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nachingwea ambaye pia ni Afisa Mipango, Joshua Mnyang’ali, alikiri kuwepo kwa mapungufu hayo na kumuomba Mkuu wa Wilaya radhi.
Hata hivyo, DC Moyo alisisitiza kuwa suala hilo halitaishia kwa maneno, bali litaamuliwa na ofisi za TAKUKURU kwa mujibu wa sheria.
Mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Nammanga umeidhinishiwa zaidi ya shilingi milioni 200, na unatarajiwa kukamilika ifikapo Februari 2026.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED