Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, leo ameanza kampeni Kigoma, mkoa maarufu ‘Mwisho wa Reli’ kunadi sera na ilani ya uchaguzi CCM, ili kusaka kura za heshima kwa chama hicho.
Ataanza kunadi sera zake wilayani Uvinza kisha kuendelea Kasulu na baadae Buhigwe, huku wananchi wa Kanda hiyo ya Magharibi wakimngoja kwa shauku kumsikiliza. Mkoa huo unatajwa kama lango la biashara na kitovu cha historia ya usafiri wa reli nchini.
Historia yake ndefu imejikita kwenye Ziwa Tanganyika, ambalo linashika nafasi ya pili duniani kwa kuwa na kina kirefu cha maji, hutegemewa kwa shughuli za uvuvi na biashara za kimataifa kwa miongo mingi.
Mkoa huo umepata umaarufu wa kipekee kama mwisho wa reli baada ya reli ya Kati (Central Line) kufika Kigoma Februari 1914, hatua iliyofungua ukurasa mpya wa usafirishaji wa watu na mizigo kutoka Dar es Salaam hadi Magharibi mwa nchi.
Katika kufungua njia za kibiashara kuelekea nchi jirani za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, serikali inatekeleza mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Tabora hadi Kigoma, hatua itakayorahisisha usafirishaji wa abiria pamoja na mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam.
Mradi huu pia unatarajiwa kuongeza ufanisi wa usafirishaji, kupunguza gharama za biashara na kuchochea ukuaji wa sekta za kilimo, uvuvi na viwanda vidogo mkoani Kigoma, huku pia ukitoa ajira kwa wananchi hususani vijana.
Kiuchumi, maisha ya wananchi wa Kigoma yamejikita katika kilimo, ambapo mazao kama mahindi, maharagwe, mihogo na matunda mbalimbali huzalishwa kwa wingi.
Kilimo kinachangia zaidi ya asilimia 70 ya ajira za wakazi wa mkoa huu.
Uvuvi katika Ziwa Tanganyika nao ni uti wa mgongo wa kipato na lishe, huku samaki aina ya migebuka na dagaa wakiuzwa ndani na nje ya nchi.
Aidha, biashara imeimarika kutokana na ukaribu wa Kigoma na nchi jirani za Burundi na Kongo, hali inayoufanya mkoa huu kuwa kitovu cha usafirishaji na masoko ya mipakani.
Utalii pia ni sehemu muhimu ya uchumi wa Kigoma kupitia Hifadhi za taifa za Gombe na Mahale, zinazojulikana kwa sokwe wakubwa (chimpanzee), huwakusanya watalii kutoka pande zote za dunia.
Aidha, historia ya Ujiji, mahali alipowasili mtafiti maarufu David Livingstone, inabaki kuwa kivutio cha kihistoria kinachokumbusha nyakati za karne ya 19.
Kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Mkoa wa Kigoma una jumla ya wakazi 2,470,967, ambapo wanaume ni 1,186,833 na wanawake ni 1,284,134.
Idadi hii inaifanya Kigoma kuwa miongoni mwa mikoa yenye ongezeko kubwa la watu, na hivyo kuongeza mahitaji ya huduma za kijamii, miundombinu na fursa za kiuchumi, ambazo leo jicho la wakazi hao wamelielekeza kwa Dk. Samia.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED