Makandarasi nchini wametakiwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zote zinazohusu shughuli za ujenzi, ikiwemo kusajili miradi wanayotekeleza, sambamba na kuepuka kukubali majina ya kampuni zao kutumika kiholela na kampuni zisizokidhi vigezo.
Kauli hiyo imetolewa na Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Mhandisi Rhoben Nkori, wakati akifunga mafunzo maalumu ya siku tatu ya Utawala Bora (Corporate Governance) yaliyofanyika jijini Mwanza mwishoni mwa wiki.
Mhandisi Nkori alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwaongezea makandarasi ujuzi na maarifa ya namna ya kutekeleza miradi ya ujenzi kwa ufanisi na viwango vinavyohitajika.
“Kupitia mafunzo haya ninaamini mmejifunza mambo mengi yatakayowasaidia katika kazi zenu. Ni muhimu kujiwekea utaratibu wa kupata elimu endelevu ili kuongeza uwezo wenu wa kutekeleza miradi kwa ubora mkubwa,” alisema.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa makandarasi kulinda hadhi na heshima ya taaluma ya ukandarasi kwa kufuata sheria na taratibu.
“Tusiruhusu mtu yeyote kuvunja sheria na kuchafua taswira ya sekta hii. Tukiona mmoja wetu anaenda kinyume, ni wajibu wetu kumshauri na kumsaidia badala ya kumruhusu kuiharibia tasnia nzima,” aliongeza.
Mhandisi Nkori pia alionya dhidi ya tabia ya baadhi ya makandarasi kukubali kurubuniwa kwa fedha ili majina ya kampuni zao yatumiwe katika vibao vya miradi kinyume na taratibu, akisema kitendo hicho kinashusha hadhi ya makandarasi.
Alibainisha kuwa sekta ya ujenzi si rahisi, bali inahitaji weledi na umakini mkubwa ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ubora, muda na kwa viwango vinavyostahili.
Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo walisema wamepata nafasi ya kubadilishana uzoefu na maarifa kuhusu mbinu mbalimbali za ujenzi, jambo litakalowawezesha kuendana na mabadiliko ya teknolojia katika sekta hiyo.
Mafunzo hayo yalihudhuriwa na makandarasi kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED