Samia: Mapambano ya uhuru wa kiuchumi yanaendelea

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 06:41 PM Sep 12 2025
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan.
Picha: CCM
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan.

Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania imepata uhuru wa kisiasa mwaka 1961 na sasa inaendelea na mapambano ya kupata uhuru wa kujitegemea kiuchumi.

Ametoa kauli hiyo leo Septemba 12, 2025, akihutubia maelfu ya wananchi waliofurika katika Uwanja wa Nanenane, mkoani Tabora, wakati wa mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu.

Dk. Samia amesema serikali inalenga kujenga taifa linalojitegemea na kuzingatia ustawi wa kila Mtanzania, kwa kuendeleza misingi aliyoisisitiza Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

“Wananchi ni sisi sote kwa pamoja, maendeleo ni juu yetu wenyewe, na maendeleo tunayoyataka ni maendeleo ya watu yaletwe na watu wenyewe, yaendelezwe na watu wenyewe, yawafuate watu kule waliko. Hii ndiyo maana halisi ya uchumi jumuishi. Tunataka kujenga uchumi jumuishi unaoleta maendeleo mijini na vijijini,” amesema.

Akiendelea, Dk. Samia amesema Mkoa wa Tabora una nafasi ya kipekee katika historia ya kisiasa ya Tanzania, kwa kuwa mmoja wa waasisi na Mwenyekiti wa kwanza wa CCM, Mwalimu Julius Nyerere, alisoma mkoani humo na baada ya kuhitimu Makerere, Uganda, alirudi kufundisha katika Shule ya Sekondari ya St. Mary’s.

“Kuna uamuzi muhimu wa kihistoria uliofanyika Tabora mwaka 1958, wakati Mkutano Mkuu wa TANU ulipoamua kushiriki uchaguzi, jambo lililosogeza nchi karibu na uhuru wake. Haya yote yanathibitisha kwamba CCM ina historia kubwa Tabora. Mnara wa kumbukumbu wa uamuzi ule wa busara wa TANU uko hapa hadi leo, ukiwa ukumbusho wa safari yetu kuelekea uhuru wa kisiasa,” amesema.