Dk. Nchimbi atua Kaskazini, 'wadudu' wamkaribisha

By Gwamaka Alipipi , Nipashe
Published at 12:54 PM Sep 12 2025
Mgombea Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi
Picha: CCM
Mgombea Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi

Mgombea Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi, amewasili leo Ijumaa, Septemba 12, mkoani Arusha kuendelea na kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.

Dk. Nchimbi amewasili jijini Arusha baada ya kukamilisha mikutano ya kampeni katika mikoa ya Katavi na Rukwa. Mara baada ya kuwasili, alielekea wilayani Longido kwa ajili ya kufanya mkutano wa hadhara, kabla ya kuendelea na Arumeru Magharibi, na hatimaye kumalizia ratiba ya leo jioni kwa mkutano jijini Arusha.

Aidha, vijana wa makundi rika maarufu kama wadudu waliompokea kwa shangwe, wamemkaribisha kwa kumpa hakikisho la ushirikiano na sapoti ya dhati katika kipindi chote atakachokuwa mkoani humo.

Kwa mujibu wa ratiba ya kampeni, Dk. Nchimbi ataendelea na ziara zake katika mikoa ya Kaskazini, akifanya mikutano mbalimbali katika mikoa ya Kilimanjaro na Tanga.

Katika mikutano yake, Mgombea Mwenza huyo amekuwa akiinadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kipindi cha 2025-2030, ambayo inalenga kuboresha maisha ya wananchi na kuimarisha maendeleo ya taifa katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Vilevile, amewataka wananchi kuendelea kumuunga mkono Mgombea Urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, pamoja na wagombea ubunge na udiwani wa chama hicho, ili kwa pamoja kuhakikisha utekelezaji wa Ilani hiyo unafanikiwa ipasavyo.