Matumizi ya nishati safi ya kupikia yaongezeka nchini – Nishati

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:36 PM Sep 12 2025
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini yameongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi asilimia 20.3 mwaka huu, huku serikali ikilenga kufikia asilimia 80 ndani ya kipindi cha miaka 10 ijayo.

Mhandisi Mramba aliyasema hayo Septemba 12, 2025 jijini Dar es Salaam, wakati akizindua Kongamano la Nishati Safi ya Kupikia lililoandaliwa na kampuni ya Mwananchi kwa ushirikiano na Wizara ya Nishati pamoja na wadau mbalimbali, likibebwa na kaulimbiu: “Nishati Safi ya Kupikia: Okoa Maisha, Linda Mazingira.”

Akizungumza katika uzinduzi huo, alisema matumizi ya nishati safi ya kupikia si jambo la kinadharia bali yanahusu maisha, mazingira na uchumi wa taifa. “Msingi wake mkuu ni kulinda afya, mazingira na maendeleo jumuishi,” alisisitiza.

Aidha, alihimiza Watanzania kuachana na matumizi ya kuni na mkaa, akibainisha kuwa takribani watu 33,000 hufariki kila mwaka kutokana na maradhi ya mfumo wa kupumua yanayosababishwa kwa kiasi kikubwa na moshi unaotokana na nishati isiyo safi.

Mhandisi Mramba alisema kutokana na changamoto hizo, serikali chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeandaa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia 2024–2034, uliozinduliwa Mei 2024, ambao unalenga kuwezesha asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Alimalizia kwa kumshukuru Rais Dk. Samia akimweleza kama kinara wa nishati safi ya kupikia kitaifa na kimataifa, kutokana na dhamira yake thabiti ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata nishati salama, nafuu na rafiki kwa mazingira.