Manabii na Mitume wazionya mamlaka zinazo simamia uchaguzi mkuu

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 04:16 PM Sep 12 2025
Manabii na Mitume wazionya mamlaka zinazo simamia uchaguzi mkuu
PICHA:PAUL MABEJA
Manabii na Mitume wazionya mamlaka zinazo simamia uchaguzi mkuu

UMOJA wa Mitume na Manabii Tanzania, umezitaka mamlaka zinazosimamia Uchaguzi Mkuu 2025, kutenda haki ili kuendelea kulinda amani na utulivu uliyopo nchini.

Rais wa Umoja huo Nabii Dk. Joshua Mwatyala, ametoa ombi hilo jana jijini Dodoma, alipokuwa akizungumza na waandishi kuhusu umuhimu wa kuendelea kuliombea taifa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Otoba 29 mwaka huu.
Amesema, ili kuendelea kulinda amani na utulivu uliopo nchini hususan kipindi hichi cha kuelekea uchaguzi mkuu, mamlaka zinazohusika kusimamia mchakato huo zinapaswa kutenda haki na kuepuka upendeleo.
“Wito wetu ni kwa wananchi wote nchini kujitokeza kwenda kupiga kura ili kuwachagua viongozi ambao wanaona watawaongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano tano, lakini rai yetu kama viongozi wa kiroho ni kuwa mamlaka zinazohusika zinapaswa kutenda haki,”amesema
Aidha, amesema kwa mgombea yeyote atakaye shinda basi atangazwe mshindi na atake shindwa asubiri tena baada ya miaka mingine mitano na siyo kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani na utulivu ulipo nchini.
“Pia baada ya matokeo kutangazwa kusiwepo na mtu yeyote ambaye atahamasisha machafuko bali watu wote tumshukuru Mungu kwa kiongozi ambaye atakuwa ametuchagulia kuliongoza Taifa letu,”amesema
Kadhalika, amesema hivi sasa kumekuwepo na utabiri mwingi kuhusu uchaguzi mkuu mwaka huu, ambapo kila mtu amekuwa akitoa mtazamo wake hali ambayo inachanganya wananchi.
“Kila mtu anatabiri uchaguzi huu utakuweje wapo, manabii, waganga, wachambuzi wanatabiri uchaguzi huu lakini sisi tunasema kuwa uchaguzi mkuu mwaka huu utamalizika salama kabisa na baada ya uchaguzi huo kila mtu akafanye kazi ili kuendelea kulijenga taifa letu,”amesema
Hata hivyo, aliwasihi wananchi kutoshawishika kujiingiza kwenye vitendo vya uvunjifu wa amani katika kipindi chote cha uchaguzi mkuu mwaka huu.