Chama cha Sauti ya Umma (SAU), kimesema kimejinasibu kutwaa majimbo 160 na kata 218 katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa Oktoba mwaka huu, kimeweka wagombea katika maeneo yote ambayo kinakubalika.
Makamu Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Simon Bayo amesema katika majimbo 272 ya uchaguzi, SAU inakubalika katika majimbo 160, na kwamba chama chao kitatwaa majimbo mengi zaidi.
Bayo amesema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na gazeti hili kuhusu mikakati na kampeni za chama hicho katika mikoa mbalimbali, zinazotarajiwa kuanza wiiki ijayo.
Amesema wao hawajaingia katika uchaguzi kienyeji, bali wamejipanga na kuchambua majimbo na kata hadi kupata idadi hiyo ya wagombea ambao chaam kinaamini watakiwakilisha vizuri.
"SAU inatarajia kuzunguka mikoa yote ambayo imeweka wagombea kuanzia Septemba 17 na tuna uhakika tutashinda, kwa sababu tumeangalia maeeno ambayo tunakubalika," amesema Bayo.
Ametaja baadhi ya mikoa hiyo kuwa ni Mara ambako wameweka wagombea ubunge katika jimbo mawili ya Tarime Mjini na Bunda Mjini na pi mikoa ya Mwanza, Pwani, Dodoma, Morogoro na Geita.
"Mikoa mingine ni Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Shinyanga, Simiyu, Kigoma, Tanga, Unguja na Pemba. Tuna uhakika na maeneo hayo, halafu tuna ilani nzuri inayogusa sekta zote," amesema.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Shaban Kirita, alitaja baadhi ya mambo mazuri yaliyomo katika ilani ya chama hicho ni ajira mpya milioni 10 ambazo zitapatika katika awamu ya kwanza ya uongozi wa SAU.
"Iwapo wananchi watakipa ridhaa chama chetu, mgombea urais, Majalio Kyara ameshasema ndani ya miaka mitano ya uongozi wake, atatoa ajira hizo, kwai uwezekano upo,tatizo ni kukos usimamizi," amesema Kirita.
Kirita amesema chama hicho kina ufumbuzi wa tatizo ambao umo ndani ya ilani yao, na kwamba kinachotakiwa ni wananchi kukipa ridhaa Oktoba 29 ili kiweze kutekeleza ahadi ambazo kimeahidi.
"Ilani yetu ina mtiririko wa ahadi za chama kwa wapigakura na Watanzania wote. Inaonyesha dira, maadili, sera na mipango ya chama katika kipindi cha miaka mitano ya utawala na kwa jinsi gani tutaweza kuwatumikia watu, kuboresha ubora wa maisha yao," amesema.
Amesema wao wanatarajia kujenga taifa ambalo linafanya kazi kwa ajili wote, taifa ambalo hakuna mtu aliyeachwa nyuma, na kwamba wana uhakika kwa pamoja nchi itafika mbali.
"Watanzania waje kwenye mikutano yetu ya kampeni wajipatie nakala ya ilani waisome na kuitafakari kwa kina ili wafanye uamuzi wa kuchagua mgombea urais wetu, wabunge, wawakilishi na madiwani," amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED