Jumla ya watu 29,743 walifariki nchini mwaka 2022 kutokana na ugonjwa wa saratani, vifo ambavyo kwa kiwango kikubwa vimesababishwa na kuchelewa kuanza matibabu hospitalini.
Takwimu hizo zilitolewa na Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Saratani wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa (BMH), Dk. Jesse Kashabano, wakati wa maadhimisho ya Mwezi wa Saratani ya Tezi yaliyofanyika jijini Dodoma.
Dk. Kashabano alisema katika kipindi hicho jumla ya wagonjwa 49,931 waligundulika kuwa na aina mbalimbali za saratani na kuanza kupatiwa matibabu. Hata hivyo, alibainisha kuwa idadi kubwa ya wagonjwa huwasilisha hospitalini wakiwa hatua ya mwisho (stage four), jambo linalopunguza uwezekano wa kupona.
“Naomba jamii ijenge tabia ya kupima afya mara kwa mara kwa sababu ni muhimu kujua mapema kama una saratani, ili upate matibabu haraka hospitalini kabla ugonjwa haujafikia hatua ya mwisho,” alisema Dk. Kashabano.
Alisisitiza kuwa saratani ni tatizo la kimataifa linaloweza kutibika iwapo mgonjwa atawahi kufika hospitali. “Saratani inatibika na mgonjwa anaweza kupona kabisa na kuendelea na maisha yake ya kawaida, mradi tu anawahi matibabu,” aliongeza.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa BMH, Dk. Henry Humba, aliishukuru taasisi ya Jema Foundation kwa msaada wa vifaa vya matibabu na elimu kuhusu saratani. Alitoa wito kwa jamii kuachana na mila na imani potofu zinazowafanya wagonjwa kuchelewa kupata huduma hospitalini.
Dk. Humba aliongeza kuwa tofauti na miaka ya nyuma ambapo matibabu ya saratani yalipatikana zaidi katika Taasisi ya Saratani Ocean Road jijini Dar es Salaam, kwa sasa huduma hizo zimesogezwa karibu na wananchi kupitia vituo na hospitali mbalimbali nchini. Aidha, hospitali hiyo imezindua ujenzi wa kituo mahiri cha mafunzo ya saratani kwa lengo la kuongeza ufanisi wa tiba na tafiti.
Naye Mkurugenzi wa Jema Foundation, Jema Baruani, aliwataka wananchi kuachana na dhana potofu kuwa saratani haitibiki. Alieleza kuwa yeye mwenyewe aliugua saratani akiwa na umri wa miaka 31 na baada ya kupata tiba, amepona na sasa ni balozi wa kuhamasisha jamii kujitokeza kupima afya na kuanza matibabu mapema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED