Mgogoro wa ardhi umeibua taharuki katika Kijiji cha Bwakila Chini, wilayani Morogoro, baada ya wananchi kufunga ofisi ya kijiji wakipinga kuuza ekari 207 za ardhi kwa mwekezaji wa kampuni ya Morogoro Sugar.
Wananchi hao wanadai hawakushirikishwa katika mkataba uliosainiwa mwaka 2018, na kwamba mikutano ya kijiji haijafanyika ili kujadili mapato, matumizi na mustakabali wa mashamba yao. Wamesema walishangazwa kupata taarifa kwamba mwekezaji alikabidhiwa eneo hilo mwaka 2021, huku wao wakijulishwa rasmi mwaka 2025.
“Tunamuomba Rais Samia aingilie kati. Viongozi wa chini wametusaliti. Tunaomba ama aje mwenyewe au amtume Waziri Mkuu, Waziri wa TAMISEMI, Waziri wa Ardhi au Mkuu wa Mkoa aje kutusikiliza kwa kina,” alisema mmoja wa wakazi wa kijiji hicho.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Bwakila Chini, Hemedi Mvunyo, alipoulizwa kwa njia ya simu alikanusha madai hayo akisema mikutano ya kijiji hufanyika kila robo mwaka. Aliongeza kuwa mkutano mwingine utafanyika muda wowote kuanzia sasa, ambapo mwekezaji ataalikwa kutoa ufafanuzi kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro amesema tayari ametoa maelekezo ofisi ya kijiji ifunguliwe na huduma ziendelee kama kawaida, huku akisisitiza kuwa tuhuma zinazohusu mkataba huo zinaendelea kuchunguzwa na ofisi yake.
Wakati huo huo, taarifa kutoka kijijini humo zimedai kuwa watu kadhaa wamekamatwa na polisi na kupelekwa mjini Morogoro kwa tuhuma za kushiriki katika kufunga ofisi ya kijiji.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED