Fredy Lowassa: Uteuzi umeisha, CCM tuwe kitu kimoja

By Gwamaka Alipipi , Nipashe
Published at 02:03 PM Sep 12 2025
Aliyekuwa Mbunge wa Monduli kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Fredy Lowassa.
Picha: Mtandao
Aliyekuwa Mbunge wa Monduli kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Fredy Lowassa.

Aliyekuwa Mbunge wa Monduli kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Fredy Lowassa, amewataka wanachama wa chama hicho mkoani Arusha kuungana, kuacha makundi na kuelekeza nguvu zao katika kutafuta kura za rais, wabunge na madiwani wa CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Fredy, ambaye ni mtoto wa Waziri Mkuu Mstaafu, Hayati Edward Lowassa, alitoa kauli hiyo leo, Septemba 12, wilayani Longido katika mkutano wa kampeni za CCM ambapo Mgombea Mwenza wa Urais, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, anatarajiwa kuinadi Ilani ya chama na kuomba kura kwa wananchi.

Amesema mchakato wa kura za maoni na uteuzi wa wagombea ndani ya CCM umeshakamilika, na vilevile Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imemaliza uteuzi wa wagombea, hivyo kilichosalia sasa ni kuhakikisha wagombea waliopitishwa wanashinda kwa kishindo.

“Mchakato ndani ya chama umekwisha, tumetumia haki yetu ya kuchagua. INEC nayo imemaliza. Mimi kama mwana-CCM kazi yangu sasa ni kukiombea kura CCM kipate kura nyingi na za kutosha,” amesema Fredy.

Fredy aliibuka mshindi katika kura za maoni jimboni Monduli, lakini jina lake lilienguliwa na Kamati Kuu ya CCM, na badala yake kumpitisha Isaac Copriano maarufu Kadogo kugombea ubunge wa jimbo hilo.

Amesisitiza kuwa baada ya kifo cha Rais John Magufuli, taifa liliingia katika sintofahamu, lakini Rais Samia Suluhu Hassan alipochukua kijiti cha uongozi ameiongoza nchi kwa utulivu, kuondoa makundi na kusimamia maendeleo.

“Katika uongozi wa Rais Samia, wakazi wa Monduli tumepata miradi mingi ya maendeleo ikiwemo ya maji na umeme, jambo linaloonesha dhamira ya dhati ya kuwaletea wananchi maendeleo,” amesema Fredy.