RC Manyara atoa agizo kupewa taarifa uwezeshaji biashara kila mwezi

By Jaliwason Jasson , Nipashe
Published at 05:21 PM Sep 12 2025
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga.
Picha: Jaliwason Jasson
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, ameagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani humo kumpatia taarifa za utendaji wa dawati maalum la uwezeshaji biashara kila mwezi, ili kufuatilia namna wafanyabiashara wanavyohudumiwa na changamoto zao kutatuliwa.

Sendiga alitoa agizo hilo leo, Septemba 12, wakati akizindua dawati hilo mkoani Manyara. Amesema anataka kupata taarifa za kila mwezi zitakazoonesha idadi ya wafanyabiashara waliopatiwa huduma, biashara mpya zilizoanzishwa pamoja na mchango wake katika kupanua wigo wa walipa kodi.

“Nataka nione kero sugu zinazojirudia kwa kila mfanyabiashara na namna zinavyotatuliwa. Pia nataka kwenye taarifa kuwe na mpango mkakati wa kutatua kero za wafanyabiashara,” alisema Sendiga.

Aidha, aliwataka watumishi wa TRA kutodharau malalamiko ya wafanyabiashara hata kama yanaonekana madogo, kwa kuwa kufanya hivyo kunaweza kuwafanya wahusika waogope au kushindwa kueleza changamoto zao kwa uwazi. 

Awali, Meneja wa TRA Mkoa wa Manyara, Alex Katundu, alisema lengo kuu la dawati hilo ni kushirikiana na wafanyabiashara kwa karibu zaidi na kutatua kero zao. Alibainisha changamoto kubwa zinazojitokeza ni urasimu wa usajili wa biashara, ugumu wa kupata masoko, pamoja na uelewa mdogo kuhusu umuhimu wa kurasimisha biashara.

“Dawati hili litawezesha huduma kusogea karibu, kutoa elimu na ushauri, na pia kuwaunganisha wafanyabiashara na taasisi za serikali husika,” alisema Katundu.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima (TCCIA) Mkoa wa Manyara, Musa Msuya, aliishukuru serikali kwa jitihada za kuboresha mazingira ya biashara na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na taasisi za umma.