Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida, imewataka wananchi kuchagua viongozi wasio watoa rushwa kwa sababu Uchaguzi Mkuu si mashindano ya kujihusisha na vitendo hivyo na kuwataka kutafakari miaka mitano ijayo.
Mkuu wa TAKUKURU wa Mkoa huo, Sosthenes Kibwengo alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa.
Kibwengo alisema kipindi hiki cha uchaguzi kumekuwa na vitendo vya kutoa rushwa kwa baadhi ya wagombea ili wachaguliwe kuwa viongozi Oktoba 29, mwaka huu
“Wito wangu kwa wananchi wa Singida tushirikiana kuhakikisha kwanza tunashiriki katika uchaguzi na kwenda kuchagua viongozi, lakini si kigezo cha utoaji wa rushwa kwani uchaguzi sio mashindano ya utoaji wa rushwa,” alisema.
Alisema wananchi wanatakiwa kutambua kuwa rushwa ni chanzo cha kupata viongozi wasiona maadili, wasiozingatia misingi ya haki, usawa, uwazi, uwajibikaji na uzalendo.
Kibwengo, alisema rushwa imekuwa ikidhofisha utawala bora na demokrasia na baadhi ya wananchi wenye sifa za uongozi bora kushindwa kugombea, kutoteuliwa na kuchaguliwa kwa kutokuwa tayari kujihusisha na vitendo hivyo.
“Kipindi kama hiki kunakuwa baadhi ya wananchi wanawapigia kura wale waliotoa rushwa kubwa. Hapana, uchaguzi sio mashindano ya utoaji wa rushwa bali ni fursa nzuri ya kutafakari miaka mitano ijayo,” alisisitiza.
Alionya kuwa wananchi kutambua kura zao zina thamani kubwa kwa kuwa wao ndio serikali, wanapochagua viongozi ambao wametokana na rushwa wanakwamisha maendeleo ya nchi kwasababu hawawezi kujikita kuleta maendeleo.
“Katiba yetu ibara ya nane inasema serikali itapata mamlaka kutoka kwa wananchi ambao ndio utaratibu uliowekwa kisheria ni ambao tunautumia kama nchi ambayo ni ya kidemokrasia kwa njia ya uchaguzi. Kwa hiyo kura hizo ambazo zinatuchagulia viongozi zinatengeneza serikali kuu, serikali za mitaa wanatuletea maendeleo,” alisema
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED