Majaliwa ataka tathimini uendelevu miradi ya uwezeshaji kaya maskini

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 01:25 PM Sep 12 2025
Majaliwa ataka tathimini uendelevu miradi ya uwezeshaji kaya maskini
Picha: Mpigapicha Wetu
Majaliwa ataka tathimini uendelevu miradi ya uwezeshaji kaya maskini

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameuagiza Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kuhakikisha unafanya tathmini ya kina na kuwasilisha mapendekezo kwa serikali juu ya hali ya upungufu wa kaya maskini nchini.

Majaliwa alitoa agizo hilo jijini Mwanza wakati akikagua maendeleo ya taasisi mbalimbali katika Kongamano la Nne la Ufuatiliaji, Tathmini na Ujifunzaji.

Amesema takwimu zinaonesha idadi kubwa ya kaya zimeendelea kujinasua kutoka kwenye umaskini, hivyo kuna umuhimu wa TASAF kutoa ushauri mahsusi kwa serikali, hususan pale hali ya kaya maskini inapobadilika.

“Takwimu zinaonesha wengi wamefanikiwa kuondokana na umaskini, hivyo kuna haja ya kujua tathmini yenu. Je, umaskini unaisha au la?” amehoji Majaliwa.

Aidha, Waziri Mkuu amesisitiza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anaamini katika umuhimu wa tathmini, na ametoa maelekezo kuwa zoezi hilo lifanyike kikamilifu katika kila taasisi ya umma ili kuhakikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025/2050 unaenda kwa ufanisi.

Kwa mujibu wake, hatua hiyo itahakikisha matokeo ya utekelezaji wa dira hiyo yanapimika mbele ya wananchi, huku yakilenga kuleta manufaa kwa Watanzania wote.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ufuatiliaji, Tathmini, Mifumo na Mawasiliano wa TASAF, Japhet Boaz, amesema tathmini ni nyenzo muhimu ya kubaini mwenendo wa umaskini na kuchochea juhudi endelevu za kuukabili.

“Hatuwezi kusema sasa umaskini umeisha na mpango usitishwe. Majanga yanapotokea, yanazalisha maskini wapya wanaohitaji msaada wa serikali. Ndiyo maana ni lazima juhudi ziendelee,” amesema Boaz.

Ameongeza kuwa kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, Tanzania imefanikiwa kufikia asilimia nane kati ya asilimia kumi za kaya maskini zilizobainishwa, na hivyo mpango wa TASAF unaendelea kuwa nguzo muhimu katika kuinua wananchi.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi, amesema ofisi yake kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za elimu imefanikiwa kuratibu mafunzo maalum kwa maofisa wakuu wa vitengo 781 kutoka ofisi za umma nchini.

Amebainisha kuwa mpango huo ni mkakati madhubuti wa kujenga uwezo wa kitaifa katika eneo la ufuatiliaji na tathmini, jambo ambalo serikali inalipa kipaumbele na kulithamini kwa dhati.