Mgombea Mwenza wa Urais CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi amesema faida mojawapo ya uwapo wa ndege ya mizigo ni usafirishaji wa maua na mboga kutoka mikoa ya Kaskazini kwenda nchi za ulaya.
Amesema Hayati John Magufuli alinunua ndege mpya 11 lakini Rais Samia Suluhu Hassan amenunua ndege mpya tano ikiwemo moja ya mizigo ambayo inasaidia katika biashara ambazo haziwezi kufanyika bila ya kutumia ndege ikiwemo biashara ya kuuza maua na mboga.
Balozi Dk. Nchimbi amesema hayo leo Septemba 13 mkoani Moshi wakati akifanya mkutano wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Balozi Dk. Nchimbi ameaema mikoa inayoongoza kwa biashara ya maua na mboga ni mikoa ya Kaskazini ikiwemo Kilimanjaro na Arusha.
Kadhalika, amesema idadi ya watalii wanaofika nchini wamefikia milioni tano. Lakini miaka minne iliyopita baada ya kutokea ugonjwa wa corona idadi ya watalii nchini ilishuka zaidi ya 200,000 .
"Samia alipopewa madaraka akagundua kuwa utalii unaleta idadi kubwa ya watalii na hasa wa ukanda wa Kaskazini. Pili utalii unaleta fedha za kigeni nchini na kujenga uchumi wetu. Akaona hilo siyo suala la kulichukulia kirahisi kirahisi akaamua kuvaa magwanda na kucheza filamu ya Loyal Tour ili aitangaze tena nchi yetu, " anasema Dk. Nchimbi.
Anasema mbali na kucheza filamu pia Raia Samia akashirikiana na maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na mabalozi kufanya kazi ya kuitangaza nchi na ndiyo imeleta matunda ya sasa katika sekta ya utalii na sasa Tanzania ni moja ya nchi ambayo watalii wamejaa muda wote siyo kwa vipindi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED