NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, amezitaka taasisi za umma na binafsi kuhakikisha zinafanya ufuatiliaji na tathmini ya mara kwa mara ili kujiandaa na athari zinazoweza kujitokeza, kwa kuwa tayari zitakuwa na suluhu.
Kadhalika amesema taasisi yoyote nchini ambayo inafanya kazi bila tathimini haiwezi kupata matokeo kwani ni sawa na mchezo wa mpira wa miguu usiokuwa na mwamuzi.
Dk.Biteko amebainisha hayo Septemba 12, 2025 jijini Mwanza wakati akifunga kongamano la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza (MEL) kwa niaba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla.
Amesema mtu au taasisi isiyofanya tathmini hujikuta ikishangazwa na matokeo badala ya kuyatabiri na kujiandaa mapema. “Anayefanya tathmini na ufuatiliaji, hata madhara yakitokea, yatakuwa madogo kwa sababu tayari ameona changamoto mapema na ameshaandaa majibu mkononi hivyo, Serikalini lazima tu ‘adopt’ mfumo wa kufanya tathmini tena bila kuhurumiana,” amesema.
Aidha amesema hawawezi kuridhika na kusikia habari njema pekee, bali ukweli ndio msingi wa hatua za maendeleo, hivyo kuwataka watathimini na wafuatiliaji nchini waendelee kuwa waadilifu, kuonesha mapungufu bila woga na kutangaza mazuri kwa sauti kubwa ili wananchi waone thamani ya Serikali yao.
“Mtu yeyote anayejaribu kukurudisha nyuma katika kazi ya tathmini anajua anachokifanya. Huu ni wajibu wetu na hatuwezi kurudi nyuma. Tunataka wananchi wajue kuwa Serikali yao inafanya kazi kwa uwazi na kwa usahihi,” amesema.
Amesema ni muhimu kuwa na mpango mkakati wa tathmini kwa kila wizara, idara na taasisi ili kuhakikisha maendeleo ya nchi hayazuiliwi na changamoto zisizotarajiwa.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Stanslaus Nyongo amesema licha ya kujitathimini kuwa ni gharama lakini kutokufanya tathmini na ufuatiliaji ni gharama kubwa zaidi kwa taasisi na taifa kwa ujumla.
Amesema ufuatiliaji na tathmini pia unasaidia kubaini changamoto za kiutendaji mapema, kufanya marekebisho na kuongeza uwajibikaji kwa watendaji wa sekta zote.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dk James Kilabuko akimuwakilisha Katibu Mkuu, Dk Jim Yonaz amesema kongamano hilo limehusisha wataalamu kutoka ndani na nje ya nchi hivyo kuwezesha ujifunzaji wa mambo mbalimbali.
Amesema miongoni mwa washiriki wametoka Afrika Kusini, Kenya, Uganda, Cameroon, Ghana, Ujerumani, Zambia na Zimbabwe ambapo washiriki walijifunza kupitia mada mbalimbali, mijadala ya kitaalamu, mafunzo na maonesho.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED