Samia autaja Kigoma kama mkoa wa kimkakati kiuchumi

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 04:22 PM Sep 13 2025
Samia autaja Kigoma kama mkoa wa kimkakati kiuchumi
PICHA: CCM
Samia autaja Kigoma kama mkoa wa kimkakati kiuchumi

Mgombea wa Urais wa Chama cha mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, amesema wamepeleka umeme Kigoma na kutengeneza mazingira, ili kufungua fursa za uwekezaji, ambapo mkoa huo umeanza kupata uwekezaji kwenye viwanda vikubwa.

Viwanda hivyo amevitaja vimo vya saruji na sukari na kuufanya kuwa wa kimkakati kwa uzalishaji wa sukari nchini. Amesema hayo leo Septemba 13, 2025, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kasulu, mkoani Kigoma, wakati akiendelea na ziara yake ya kampeni.

“Niahidi tunaandaa zaidi mazingira ili wawekezaji zaidi wawekeze, kwa kuwa kuna reli zinaishia Kigoma ya zamani na ya kisasa, wawekezaji watakuja kwa wingi kwa sababu usafirishaji kwenda masoko ya jirani utarahisishwa,” amesema. Amesema atakayejenga kiwanda leo miaka miwili ijayo atakuta reli imekwenda mbali zaidi na kufanya biashara.

“Kiwanda cha sukari imetengeneza ajira 500, na huu ni mwanzo tu,” amesema. Amesema mwaka 2022 waliwasha umeme wa gridi ya taifa wilayani humo na kuzima mitambo na majenereta, mradi uliookoa Sh. bilioni 58 zilizokuwa zikitumia kwa mafuta, ambazo imechangia kufikisha umeme vijijini vyote mkoani humo.
Amesema walichoamua ni kuendelea ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa maji mto Malagalasi utakaozalisha megawati 49.5 na kuwa na kituo cha kupooza umeme kitakacholeta nishati hiyo wilaya za mkoa huo, ili kumaliza kadhia upungufu wa umeme mkoani huko.