Pinda:Msidanganywe wanaotaka kuleta ubabaishaji katika amani

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 03:58 PM Sep 13 2025
WAZIRI Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda
PICHA: MTANDAO
WAZIRI Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda

WAZIRI Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda, amewasihi wananchi mkoani Kigoma wasidanganywe watu wanaotaka kuleta ubabaishaji katika masuala ya amani na utulivu wa nchi.

Pinda ambaye pia ni Mratibu wa Kampeni Kanda ya Magharibi, aliwataka Watanzania kuendelea kumshukuru Mungu kwa kuijalia nchi amani na utulivu. Amesema hayo leo Septemba 13, 2025, Mkoani Kigoma katika Kata ya Kazuramimba Wilaya ya Uvinza wakati akimwombea mgombea urais kwa Chama Cha Mapinduzi, Samia Suluhu Hassan,kura ikiwa ni mwendelezo wa kampeni za uchaguzi.

“Tunaopata bahati kwenda nchi nyingine huko ni hatari, Tanzania tuna bahati ya amani ambayo imejengwa haikudondoka, imejengwa kupitia viongozi wetu,
Dk. Samia tangu ameingia mahubiri yake sehemu kubwa ni amani na utulivu, kwahiyo nawasihi sana wananchi wa Kigoma, Uvinza msidanganywe na watu wanaotaka kuleta ubabaishaji katika masuala ya amani na utulivu wa nchi.”

Alisema bila amani na utulivu hakuna maendeleo hivyo ni vyema tunu hiyo ikatunzwa kwa nguvu zote. Pinda aliwataka wananchi wa Kigoma kuhakikisha wanatafuta kura za kishindo kwa wagombea katika uchaguzi mkuu ili waongoze.

“CCM tunachotafuta ni ushindi wa kishindo, ili watu waseme sisi ni balaa, mkitaka tupate hicho tushikamane na tuendelee kuwa wamoja.
Ukitaka kukitafuta chama nenda katika Shina, Kigoma kwa bahati nzuri mna mashina 8629, matawi 628, nakiomba chama Mkoa na Wilaya kila tawi likibeba mashina 13 tutafikia yote,”alisema Pinda.

Aliwataka viongozi hao kwenda chini katika mashina kutafuta kura za kishindo kwa chama kwakuwa ndiyo kwenye siasa na ushindi.