JAMII bado inahitaji elimu zaidi kuhusu kukabiliana na kupinga vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia pamoja elimu ya uzazi ili kuwa na taifa salama imeelezwa.
Kauli hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam na Ofisa Miradi wa Taasisi ya isiyo ya kiserikali ya Flaviana Matata Foundation (FMF), Suzan Cleophos, wakati wa warsha ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari katika kuripoti matukio hayo pamoja na kutoa elimu ya uzazi kwa vijana.
Alisema bado vitendo vya unyayasaji wa kijinsia kuanzia kwa watoto mpaka watu wazima vinatokea katika baadhi ya mikoa na hivyo elimu zaidi inahitajika ili kukabiliana navyo.
"Elimu bado inahitajika sana kukabiliana na vitendo hivi vya unyanyasaji wa kijinsia, pamoja na jitihada za Serikali na taasisi nyingine na FMF, bado kuna baadhi ya maeneo vinaendelea kutokea, tunahitaji kuunganisha nguvu na kuendelea kuelimisha jamii ili kuvipunguza na kuviondoa kabisa kwenye jamii," alisema Suzan.
Alisema taasisi hiyo inaendelea kutoa elimu katika maeneo mbalimbali na kutumia wadau kufikisha elimu kwa jamii.
"Hatuangalii tu vitendo hivi ya unyanyasaji wa kijinsia, lakini pia elimu ya uzazi kwa vijana wetu ni muhimu kukabiliana na mimba za utotoni na magonjwa kama HIV," alisema Suzan.
Alisema mpango huo wa kutoa elimu kukabiliana na vitendo hivyo kwa kiasi kikubwa unasaidiwa na 'Woman Fund Trust' (WFT).
Kwa upande wake, mwezeshaji katika warsha hiyo, Rehema Longo kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania, alisema elimu kama hizi zinasaidia kukabiliana na matendo yasiyofaa katika jamii.
"Vijana, hususani wasichana wapo kwenye wakati mgumu zaidi, elimu kama hizi zikiwafikia zitasaidia kuwapa uwelewa wa kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia, pamoja na kujua mambo ya afya ya uzazi.
"Kupitia warasha kama hizi kwa wadau ambao ni daraja la kuifikia jamii, zinasaidia sana kujenga uwelewa, tunaishukuru na kuipongeza FMF kwa kuona umuhimu huu wa elimu kwa vijana pamoja na kukabiliana na vitendo vya unyanyasaji," alisema Rehema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED