Kesi kupinga uteuzi wa Tume ya Uchunguzi yaahirishwa

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 02:03 PM Dec 10 2025
Kesi kupinga uteuzi wa Tume ya Uchunguzi yaahirishwa

Kesi Na. 30210/2025 inayowahusisha Rosemary Mwakitwange na wenzake wawili dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wajumbe nane wa Tume ya Uchunguzi ya Matukio ya Oktoba 29, 2025, pamoja na Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), ilitarajiwa kutajwa leo saa tatu asubuhi mbele ya Jaji Mtembwa katika Mahakama Kuu, Dar es Salaam.

Kesi hiyo inatokana na malalamiko ya waombaji watatu wanaopinga uteuzi wa tume hiyo inayosimamiwa na aliyekuwa Jaji Mkuu, Othman Chande.

 Waombaji wanadai kuwa tume haina uhuru wa kutosha katika utekelezaji wa majukumu yake, iliumbwa kinyume na misingi ya sheria, na kwa nia mbaya yenye malengo ya kupotosha mchakato wa uchunguzi wa matukio ya Oktoba 29. Wanasisitiza kuwa uundaji wa tume hiyo hauendani na mantiki za kisheria ikilinganishwa na mazingira ya matukio hayo.

Kupitia hati ya maombi yao, waombaji wameomba Mahakama Kuu itengue uteuzi wa tume hiyo kwa madai ya kukosa sifa za kisheria. Pia wanaitaka mahakama kuzuia mamlaka zinazohusika na uteuzi kuendelea kuunda tume yenye muundo unaolalamikiwa.

Pande zote zinatarajiwa kuwasilisha taarifa za awali wakati wa utajwa wa kesi, kabla ya kupanga utaratibu wa kusikiliza hoja za msingi. Hata hivyo, shauri hilo limeahirishwa na sasa linatarajiwa kusikilizwa tena tarehe 12 Desemba mwaka huu.