Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Musa Kilakala, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuimarisha na kulinda amani ya nchi, akisisitiza kuwa hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana bila kuwepo kwa utulivu wa kijamii na kiusalama.
Kilakala ametoa kauli hiyo wakati akifungua Maonesho ya Biashara ya Mkoa wa Morogoro (MRTFE) yanayofanyika katika Uwanja wa Jamhuri, maonesho yaliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA), kuanzia Novemba 20 hadi 30 mwaka huu. Alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima.
Amesema amani ni nguzo muhimu ya uchumi na ustawi wa Taifa, na bila yake maonesho kama hayo yanayowakutanisha wajasiriamali na wawekezaji yasingewezekana.
“Amani inapaswa kuimarishwa maana bila ya amani maonesho kama haya yenye kuleta maendeleo kwa wajasiriamali, mkoa na Taifa kwa ujumla yasingefanyika, hivyo kudhoofisha uchumi wa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla,” amesema Kilakala.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TCCIA, Oscar Kisanga, amewahamasisha wafanyabiashara kujiunga na chemba hiyo ili kunufaika na fursa mbalimbali ikiwemo huduma za masoko, upatikanaji wa mikopo, na kuunganishwa kwenye masoko ya kimataifa. Ametoa wito kwa wajasiriamali kuimarisha ubora wa bidhaa zao ili ziendane na soko la Afrika, ambalo linatarajiwa kufunguka zaidi ifikapo mwaka 2030 na kuwafungulia Watanzania fursa kutoka kwa watu zaidi ya bilioni 1.4 barani humo.
Naye Afisa Mwandamizi wa Elimu na Mawasiliano kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Morogoro, Immaculate Chaggu, amesema mwamko mkubwa wa ulipaji kodi miongoni mwa wafanyabiashara umesaidia mkoa huo kuvuka lengo la mwaka 2025 kwa zaidi ya asilimia 100.
“Kila Alhamisi tunatoa elimu kwa wateja juu ya ulipaji kodi. Mwaka huu tumekusanya zaidi ya asilimia 100, lakini bado tunasisitiza ulipaji wa kodi kwa hiari,” amesema Chaggu.
Kwa upande wake, Afisa Matekelezo kutoka Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) mkoa wa Morogoro, Mema Kabaiza, ametoa wito kwa wajasiriamali kujiunga na mfuko huo ili kunufaika na mafao muhimu kama pensheni ya uzeeni na bima ya afya, hatua itakayowasaidia kukabiliana na gharama kubwa za matibabu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED