Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amepongeza Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha kwa namna walivyosimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika kipindi cha mwaka 2024/2025.
Mkuu huyo wa mkoa pia amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Dk. Rogers Shemwelekwa, kwa usimamizi wa mapato ya ndani sambamba na ubunifu wa vyanzo vya mapato ambavyo vinaongeza makusanyo.
Kunenge ameyasema hayo leo Juni 16, 2025, wakati akizungumza kwenye kikao cha Baraza Maalum la Madiwani kwa ajili ya kujadili hoja za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kikao ambacho kimefanyika katika Halmashauri ya Mji Kibaha.
Amesema Kibaha Mjini imekuwa Halmashauri ya kuigwa kwa kuwa katika kipindi kifupi cha Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Dk. Shemwelekwa, yametokea mabadiliko ya kimaendeleo katika miradi mbalimbali.
Kunenge amesema Kibaha Mjini imefanikiwa kutekeleza miradi mingi ya kimaendeleo, ikiwa ni pamoja na ukamilishaji wa soko la kisasa la Kibaha Shopping Mall, ujenzi wa shule za mchepuo wa Kiingereza pamoja na miradi mingine mbalimbali.
Amesema Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ameonyesha ushirikiano katika utendaji na kufanikisha ongezeko la makusanyo ya mapato ya Halmashauri kutoka Sh. bilioni 4 mwaka 2023 mpaka kufikia Sh. bilioni 10 mwaka 2024, huku mwaka 2025/2026 wakitarajia kufikia mapato ya Sh. bilioni 20.
Kadhalika, ametoa wito kwa Halmashauri za mkoa huo kumsaidia Rais katika kukusanya mapato yatakayotekeleza miradi ya maendeleo badala ya kumuachia kazi ya kutafuta fedha mwenyewe.
Kunenge pia amesema hatamvumilia mtu yeyote atakayekuwa kikwazo cha kumkwamisha Rais katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku, hususani kwenye kuleta mabadiliko ya kimaendeleo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Musa Ndomba, amesema Halmashauri hiyo imefanya kazi na Wakurugenzi watatu, na kila mmoja alitimiza wajibu wake, lakini Dk. Shemwelekwa amekuwa Mkurugenzi wa mfano zaidi kutokana na kazi zake anazofanya.
Ndomba amesema ukiwa kiongozi lazima uchague vitu vya kuvifanyia kazi ili kukomesha changamoto ndogondogo zinazojitokeza sehemu ya kazi, na Mkurugenzi huyo amekuwa akifanya hivyo na kuwezesha mipango iliyopangwa kwenda kwa wakati.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED