BoT yatia saini mikataba minne ununuzi dhahabu

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 10:55 AM Jun 17 2025
BoT yatia saini mikataba minne ununuzi dhahabu.
Picha:Mpigapicha Wetu
BoT yatia saini mikataba minne ununuzi dhahabu.

Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetia saini mikataba minne ya ununuzi wa asilimia 20 ya dhahabu inayochimbwa na kusafishwa nchini, ikiwa ni hatua muhimu ya kukuza uchumi wa taifa na kuwawezesha wachimbaji madini.

Mikataba hiyo ilitiwa saini kati ya BoT na kampuni za Geita Gold Mining (GGML), Shanta Mining, Buckreef na kiwanda cha Usafishaji Dhahabu cha Geita (Geita Gold Refinery - GGR).

Akizungumza wakati wa hafla hiyo jijini hapa jana, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba alisema utiaji saini huo ni sehemu ya utekelezaji kifungu cha 59 cha Sheria ya Madini kinachowataka wachimbaji kutenga asilimia 20 ya uzalishaji kwa ajili ya masoko ya ndani, huku BoT ikipewa haki ya kwanza ya ununuzi.

"Hii ni hatua muhimu ya kimkakati kwa taifa letu. Inasaidia kuimarisha akiba ya fedha za kigeni, kuongeza thamani ya madini yetu na kuimarisha uwezo wa kiuchumi wa wachimbaji wakubwa na wadogo," alisema Dk. Nchemba.

Aliagiza kampuni za usafishaji dhahabu kuongeza uwezo wao wa uzalishaji na kufikia viwango vya kimataifa vya London Bullion Market Association (LBMA) ili dhahabu ya Tanzania iendelee kukubalika kwenye masoko ya kimataifa.

Dk. Nchemba alieleza kuwa hadi sasa BoT imenunua kilo 5,022 za dhahabu safi (sawa na tani 5.022) zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 554, kiasi kinachozidi malengo ya awali ya Dola milioni 350 kwa mwaka wa fedha 2024/25. Serikali inalenga kufikia ununuzi wa tani sita ifikapo mwakani.

Waziri wa Madini, Antony Mavunde, alisema hatua hiyo ya serikali inalenga kuongeza thamani ya madini kabla ya kuuza nje, huku akiahidi Wizara ya Madini itaendelea kuhamasisha uongezaji thamani katika sekta hiyo.

"Leo (jana) tunaandika historia. Hili ni jambo ambalo mwanzo lilionekana kuwa gumu lakini sasa limefanikiwa kwa kasi. Tuko njiani kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 10 duniani zenye akiba kubwa ya dhahabu," alisema Mavunde.

Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba alisema mpango wa ununuzi wa dhahabu ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kupunguza utegemezi wa mikopo ya nje kwa kuimarisha akiba ya fedha za kigeni kupitia sekta ya madini.

"Kupitia mpango huu, dhahabu imenunuliwa kutoka viwanda vitatu vya ndani vilivyoidhinishwa kwa bei nzuri na kwa viwango vya kimataifa. Hatujapokea malalamiko yoyote kutoka kwa wauzaji," alisema Tutuba.

Alibainisha kuwa dhahabu hiyo imehifadhiwa katika maeneo mbalimbali; kilo 162 zimo katika akaunti ya BoT iliyoko Benki Kuu ya Uingereza, kilo 2,775 katika tawi la Mwanza na kilo 719 katika tawi la Dodoma, huku kiwango kingine kikisafirishwa hivi karibuni kwenda Uingereza.

Gavana Tutuba alisema BoT inatoa malipo ya dhahabu ndani ya saa 24 baada ya ununuzi ili kuwapa wauzaji uhakika na motisha ya kuuza kwa taasisi hiyo.

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samwel Maneno, alisisitiza mkakati huo utasaidia serikali kuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni na kuongeza uwezo wa kujitegemea kifedha kwa kutumia rasilimali zilizomo nchini.

Alisema mikataba hiyo ni hatua muhimu katika utekelezaji Sera ya Madini ya kuongeza thamani ya rasilimali, kukuza mapato ya taifa na kuweka Tanzania katika ramani ya kimataifa ya biashara ya madini kwa viwango vya juu.