Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), limesema kuwa linatekeleza kwa vitendo sera ya ubia kwa kuingia makubaliano na kampuni na taasisi binafsi kwa ajili ya kujenga nyumba za kisasa na bei nafuu kwa ajili ya makazi na biashara.
Akiwasilisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo baada ya ziara fupi ya wahariri wa vyombo mbalimbali leo Juni 16, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, amesema wamelazimika kuingia kwenye PPP kwa kuwa wana ukomo wa kukopa hivyo ni lazima kutumia mitaji ya sekta binafsi.
“Kuna miradi 21 itakayotekelezwa kwa utaratibu wa PPP kati yake 17 ni Dar, mitatu Mwanza na mmoja Iringa yenye thamani ya Sh. bilioni 351. Tuna mradi wa ushirikiano na sekta binafsi katika mtaa wa Uhuru na Kongo Dar es Salaam ambao umekamilika kwa asilimia 100,” amesema Abdallah.
Aidha, NHC imewaonya wanaokwepa madeni ya pango kuwa wanajisumbua kwa kuwa NHC imejiunga na mfumo wa Credit Information Bureau ambao kwa kushirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na BRELA wanapata taarifa za mtu.
Abdallah amesema anayesumbua ataripotiwa na kupoteza sifa ya kukopesheka kwenye taasisi mbalimbali kama benki na nyingine, na kwamba dawa ya deni ni kulipa na si kukimbia.
Aidha, amesema NHC inatarajia kutumia Akili Unde (AI) na teknolojia za kisasa kwenye usalama kwa utambuzi wa wateja wake na kwamba lengo ni kubadili mtazamo wa wanaopenda nyumba za bei rahisi, bali wanunue au kupangisha kwasababu ya huduma bora.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED