Mwenyekiti Chatanda aagiza halmashauri kujenga uzio Hospitali ya Lulanzi

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 01:35 PM Jun 16 2025
Mwenyekiti Chatanda aagiza  halmashauri kujenga uzio  Hospitali ya Lulanzi
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwenyekiti Chatanda aagiza halmashauri kujenga uzio Hospitali ya Lulanzi

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT), Mery Chatanda, ameielekeza Halmashauri ya Mji wa Kibaha kuweka uzio kuzunguka Hospitali ya Wilaya ya Halmashauri hiyo (Lulanzi) ili kuepuka uvamizi ambao unaweza kutokea.

Chatanda ametoa agizo hilo Juni 15, mjini Kibaha, wakati wa ziara ya kikazi ya siku moja aliyoifanya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 pamoja na kuhamasisha wananchi kushiriki katika uchaguzi ujao.

Akizungumza mara baada ya kukagua hospitali hiyo, amesema ameridhishwa na namna Halmashauri ilivyosimamia kwa ubora ujenzi wa hospitali hiyo pamoja na huduma zinazotolewa.

Amesema hatua hiyo inaonyesha dhamira ya dhati ya Serikali ya kuboresha huduma za afya karibu na wananchi pamoja na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.

"Ilani inasisitiza afya bora, Serikali imefanya hilo kwa kuongeza hospitali za rufaa, wilaya na vituo vya afya, na hapa majengo yamejengwa kwa kiwango kizuri, mazingira yake yanavutia," amesema.

Chatanda amewataka wananchi kuepuka kusogea kwenye mipaka ya hospitali ili kuepusha kuingiza hospitali kwenye migogoro na wananchi.

Awali, akimkaribisha Mwenyekiti huyo, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson John, amesema Serikali imeendelea kuipatia Halmashauri fedha zaidi ya shilingi milioni 400 kwa ajili ya maboresho ya hospitali hiyo, ambapo kati ya fedha hizo zilitolewa kwa ajili ya kumaliza kero ya maji.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini amepongeza Serikali kwa kutoa fedha nyingi katika jimbo hilo na kutekeleza miradi ya maendeleo yote ambayo ameiomba kwa asilimia 98.

Akiwa mjini Kibaha, Mwenyekiti huyo ambaye ameambatana na wajumbe wa Sekretarieti ya UWT Taifa, wamekagua miradi mbalimbali ikiwemo Hospitali ya Wilaya (Lulanzi), soko la kisasa la Halmashauri hiyo, shule ya msingi ya Serikali mchepuo wa Kiingereza.

Miradi mingine ni pamoja na kituo cha afya Kongowe pamoja na kuweka jiwe la msingi nyumba za watumishi wa chama hicho Kibaha Mjini.