Shiriki la Nyumba la Taifa (NHC), limesema faida inayopatikana kwenye nyumba za bei kubwa inatumika kuwekeza kwenye nyumba za bei nafuu kwa ajili ya Watanzania wa kipato cha chini kuwa na makazi bora na salama.
Aidha, limeeleza kwanini mradi wa Samia Housing Scheme eneo la Tanganyika Packers Kawe, Dar es Salaam umepewa jina hilo kuwa ni kuenzi mchango wake kwenye mageuzi ya NHC kwa kuruhusu wakope kwenye taasisi za fedha na kukamilisha miradi mitatu iliyokwama kwa miaka minane na kusababisha hasara na mzigo kwa wapangaji.
Akiwasilisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo baada ya ziara fupi ya wahariri wa vyombo mbalimbali, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, amesema Shirika hilo linatekeleza miradi ya uboreshaji wa miji kwa kuvunja majengo ya zamani na kuyajenga upya, vitovu vya miji (satellite city) kwa kuendeleza maendeleo ya miliki, miradi ya ubia na uendelezaji miliki, na nyumba za gharama kubwa.
“Kutokana na mabadiliko ya sera yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan tuna nyumba za kupangisha kuanzia Sh. milioni 50 hadi 900, na zote zimeshapata wapangaji kabla ya mradi kukamilika, kwasasa shirika linapata faida na hiyo tunairejesha kwa jamii kwa kujenga nyumba za bei nafuu ambazo watanzania wa kipato cha chini watamudu,” amesema.
Abdallah amesema wanabuni na kujenga miradi mbalimbali katika miji na majiji, na kwamba asilimia 75 ya biashara iko Dar es Salaam yenye mikoa ya NHC mitano, huku ukuaji wa faida ya shirika ukiwa ni kutoka Sh. bilioni 198 miaka mitano iliyopita hadi 235 mwaka huu.
Mkurugenzi huyo amesema shirika hilo linajenga nyumba 5,399 za Sh. bilioni 659.48 kwa ajili ya kuuza na kupangisha, nyumba 3,217 zimekamlika na 2,182 ziko katika hatua mbalimbali na ujenzi wake utakamilika Juni 2026.
Kuhusu nyumba za bei nafuu za Samia Housing Scheme (SHS) amesema, nyumba 5,000 za gharama za kati na chini kwa ajili ya kuuza na kupangisha, ikiwa ni namna ya kurejesha shukrani kwa Rais Samia kwa kufanya mabadiliko ya kisera kwa shirika hilo na sasa linaweza kukopa.
“Kutokana na kuikwamua miradi mitatu ya Kawe 711, Morocco Square na Samia Housing Scheme ambayo Rais alitukwamua, tuliwaza sisi tunamlipa nini, tukagundua nyuma ni namna sahihi ya kumlipa kwa kuwa na miradi mitatu ya nyumba za bei nafuu za Dar es Salaam, Dodoma na maeneo mbalimbali nchini.“Nyumba hizo asilimia 50 zitajengwa Dar, asilimia 30 zitajengwa Dodoma 30 na 20 maeneo mbalimbali nchini. Samia Housing Scheme Tanganyika Packers kuna nyumba 560 ambazo zimeshauzwa mwaka mmoja uliopita. Hii ni tafsiri ya uchumi wetu unakuwa vizuri. Rais Samia atazizindua mwezi ujao,” amesema.
Aidha, amesema baada ya mradi wa Tanganyika Packers kukamilika watajenga katika eneo la Kijichi, Medeli Dodoma na kwamba gharama ni nafuu ambazo Watanzania wa kipato cha kati wanaweza kununua, pamoja na za bei ndogo bila kuathiri ubora.
“Namna pekee ya kuleta utulivu kwenye miji na majiji ni kuwa na makazi bora, nchi inayowekeza kwenye makazi huwezi kukuta watu wakiandamana barabarani, tuna kiongozi (Rais) anayetaka kuona mabadiliko nasi tunaitumia fursa vizuri, alituelekeza tujenge makazi kwa ajili ya kada za chini kama walimu na wengine nasi tumejenga na tunajenga,” amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED