Waliopigana Vita ya Kagera waomba kulipwa pensheni na kifuta jasho

By Christina Haule , Nipashe
Published at 05:23 PM Jul 08 2025
Askari mgambo Ally Salum (69) akionesha baadhi ya nyaraka alizofikisha ofisi ya mkuu wa mkoa kuomba kusaidiwa kupata fidia.

Baadhi ya askari wa ulinzi wa Jeshi la Mgambo waliokuwa wakilitumikia Taifa kupitia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakati wa Vita ya Kagera, wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan, kuwaangalia kwa jicho la huruma na kuwaingiza kwenye mpango wa malipo ya pensheni na kifuta jasho kama ilivyo kwa maveterani waliotangazwa hivi karibuni kuanza kulipwa.

Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro, askari hao wamesema licha ya kuhusika moja kwa moja katika vita hiyo muhimu ya kulinda mipaka ya nchi, hawakuwahi kupata stahiki zozote hadi leo, huku wenzao wakitangazwa kufaidika na mpango wa serikali unaotarajiwa kuanza Julai 2026.

Mmoja wa askari hao ni Vaileth Lukonge (64), mkazi wa Mafiga, Morogoro, ambaye amesema aliitumikia nchi kupitia Jeshi la Mgambo kwa moyo mmoja, lakini hadi sasa anaishi maisha ya shida bila kutambuliwa rasmi kama mstaafu au mzalendo aliyetoa mchango wake katika ulinzi wa taifa.

“Nilijiunga na Jeshi la Mgambo mwaka 1977 kupitia chuo cha Mikumi nikasomea kozi ya miezi mitatu, kisha nikaenda Dar es Salaam kusomea Jeshi la Anga kwa miezi sita. Niliambiwa nikimaliza kozi ya miaka mitatu ningeajiriwa, lakini sikukubali kwa sababu ya mazingira magumu niliyokutana nayo,” amesema Lukonge.

Ameeleza kuwa changamoto za kijinsia na ukali wa mafunzo zilipelekea kushindwa kuvumilia hadi mwisho wa utaratibu wa ajira ya kudumu, lakini bado alihudumu ipasavyo kama mgambo kwa wakati wake.

Naye Ally Salumu Mbiki (69), mkazi wa Kata ya Mjimpya Manispaa ya Morogoro, amesema alianza kulitumikia Taifa akiwa na umri wa miaka 22, ambapo mwaka 1979 alitumwa vitani Kagera akiwa kama mkufunzi wa FFU waliokuwa wakijiunga na vikosi vya kupambana na adui. Alifundisha mbinu za ukakamavu na matumizi ya silaha kwa wanajeshi waliokuwa wakipelekwa Makutopora kabla ya kwenda mstari wa mbele.

“Tulipomaliza vita, nilipata tu fulana yenye maandishi ‘ahsanteni wanajeshi wetu’, lakini hakuna kifuta jasho wala pensheni hadi leo. Nimeendelea kuishi kwa shida, nikihangaika na watoto katika kituo cha malezi nilichojiunga nacho baadaye, lakini hali ya afya yangu ilianza kudorora,” amesema Mbiki kwa masikitiko.

Askari hao wamesema wanakumbushia ombi lao kwa Rais Samia kutokana na matumaini yaliyowekewa na serikali kwa maveterani wa JWTZ, huku wakiamini na wao pia walihusika moja kwa moja katika operesheni hiyo ya kihistoria.

Hivi karibuni, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Tax, akijibu swali bungeni, alisema serikali imeanza hatua za kuwaingiza maveterani waliopigana vita ya Kagera kwenye mpango wa pensheni kuanzia Julai 2026, kwa kiwango cha chini cha pensheni ya JWTZ ambacho kitaendelea kupanda kulingana na mabadiliko ya viwango.