Serikali imezindua rasmi Programu Maalum ya Samia Extra Scholarship kwa ajili ya masomo ya Sayansi ya Data (Data Science), Akili Bandia (Artificial Intelligence) na Sayansi Shirikishi (Interdisciplinary Science), ikiwa ni hatua ya kimkakati ya kuijenga Tanzania ya uchumi wa maarifa unaoongozwa na vijana wabunifu na wenye vipaji vikubwa.
Uzinduzi wa programu hiyo umefanyika leo katika Chuo cha Nelson Mandela cha Sayansi na Teknolojia ya Afrika (NM-AIST) kilichopo jijini Arusha, na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wawakilishi wa taasisi za elimu na wadau wa maendeleo ya teknolojia.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Makamu wa Rais wa NM-AIST, Profesa Maulilo Kipanyula, amesema ni fahari kwa chuo hicho kushiriki moja kwa moja katika maandalizi ya kizazi kipya cha wataalamu wa teknolojia duniani.
“Tunashukuru Wizara na Serikali kwa kukiamini chuo hiki kama kitovu cha maandalizi kwa wanafunzi hawa. Kwa kweli tunajivunia kuwa sehemu ya historia ya kujenga taifa la wataalamu wa data science na AI,” amesema Profesa Kipanyula.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk. Amos Nungu, amesema programu hiyo ni zaidi ya mpango wa masomo kwani ni tamko la kitaifa la kujenga taifa lenye msingi wa maarifa na uvumbuzi wa kiteknolojia.
“Tunachofanya leo si tu kutoa ufadhili wa masomo; huu ni uwekezaji wa kizalendo utakaowezesha vijana wetu kuwa sehemu ya mapinduzi ya nne ya viwanda,” amesema Dk. Nungu.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema programu hiyo ni utekelezaji wa ahadi ya kukuza matumizi ya Akili Bandia kama ilivyoainishwa kwenye bajeti ya mwaka 2025/2026.
“Kwa mara ya kwanza, si uwezo wa familia yako unaoangaliwa, bali uwezo wa akili yako,” alisema Prof. Mkenda na kusisitiza kuwa:“Ukiwa miongoni mwa walioteuliwa, usiombe chuo kingine mwaka huu. Njoo NM-AIST uandaliwe kwa miezi 10, utapewa kompyuta, kufundishwa kozi ya awali na kuandaliwa kwa maisha ya kimataifa.”
Katika awamu ya kwanza, wanafunzi 700 bora kutoka kwenye matokeo ya mitihani ya taifa watateuliwa. Kati yao, 50 waliofanya vizuri zaidi katika tahasusi ya Sayansi na Hisabati ya Juu watapelekwa vyuo bora vya kimataifa kama Massachusetts Institute of Technology (MIT) Marekani, Chuo Kikuu cha Oxford (Uingereza), IIT Madras (India), na Peking (China).
Wanafunzi wengine 650 watasoma ndani ya nchi kwa ufadhili kamili wa serikali.
“Hatuwezi kujifungia. Lazima tukafuate elimu popote ilipo, tunataka vijana wetu wakachote maarifa huko na walete nyumbani,” amesisitiza Prof. Mkenda.
Programu hiyo ni ushirikiano kati ya NM-AIST, COSTECH, Wizara ya Elimu, wataalamu wa diaspora na taasisi za kimataifa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kuiweka Tanzania katika ramani ya maarifa ya dunia.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED