WIZARA ya Nishati kwa kushirikiana na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Umoja wa Ulaya (EU) wamezindua programu ya ushindanishwaji kwa wabunifu katika sekta ya nishati, wakilenga kuchochea mpango wa matumizi bora ya nishati.
Imeelezwa kuwa katika ushindanishwaji huo watatafutwa washindi 10 ambao watakuwa na miradi inayochochea matumizi sahihi ya nishati na kuleta suluhu ya changamoto mbalimbali za kijamii katika sekta hiyo, na kwamba kila mshindi atapatia Sh. Milioni 25 hadi 30 kama mtaji wa kuendeleza mradi wake.
Akizungumza leo mkoani Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa program hiyo awamu ya pili, Mwakilishi wa UNDP anaeshughulikia mabadiliko ya tabianchi na nishati, Abas Kitogo, amesema ushindanishwaji huo unahusisha wabunifu wa ndani pekee.
“Watanzania wabunifu wenye teknolojia wanazotaka kuziendeleza wasikose fursa hii, kutafanyika mchakato wa wazi na watakaofanikiwa kupita 20 watapatiwa mafunzo maalum katika kuendeleza bunifu zao, mwaka huu tutaangalia maeneo matatu ikiwemo kuongeza ubunifu katika matumizi bora ya nishati kwenye majengo.
“La pili ni teknolojia ya kuongeza ubora wa vifaa vya nishati vitumike kwa usahihi zaidi, pia teknolojia ya ubunifu kuhusu usambazaji wa taarifa za matumizi sahihi ya nishati katika kubadilisha tabia za watu katika jamii na kuwafanya wawe na uelewa kuhusu matumizi bora,” amesema Kitogo.
Emilian Nyanda, aliyemuwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, amesema mpango wa matumizi bora endelevu ya nishati nchini imesaidia kwa asilimia kubwa kupata nishati ya bei nafuu, utunzaji wa mazingira na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Naye, Neema Walter, ambaye ni mwanzilishi wa kampuni ya Nishati Next Technology, amesema katika mafunzo waliyopatiwa alifanikiwa kupata ufadhili, pamoja na maarifa yak umuwezesha kuzalisha mashine za kuchakata plastiki, pamoja na majiko.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED