MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, ameishauri serikali kupitia Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) kuwa karibu na wawekezaji wote wakiwemo wakubwa, wa kati na wa chini ili kuongeza kasi ya kukuza uchumi.
Wasira ameyasema hayo leo alipotembelea Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa Saba Saba yanayoendelea mkoani Dar es Salaam.
Amesema TISEZA ni muhimu katika uchumi wa Tanzania kwa kuwa ndio inayosajili, kuwatia moyo na kuwaelekeza wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali.
“Wizara ya Kilimo inafanya jitihada ya kuongeza uzalishaji, inatoa mbolea ya ruzuku kwa wakulima waweze kuzalisha zaidi lakini hiyo haitoshi, kama tukipata wawekezaji wa ndani wa kuongeza thamani ya mazao yao,” amesema.
“Ili tutoke hapo lazima twende katika viwanda vya nguo sio lazima viwe vikubwa, ukienda India kuna viwanda vidogo vingi sana mmoja anatengeneza nyuzi na anamuuzia anayetengeneza nguo, kwa kufanya hivi tutafanya kilimo kuwa na soko la uhakika na kushusha umasikini,” amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED