Katibu Mkuu azipongeza PURA na ZPRA

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 06:50 PM Jul 08 2025
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Captain Hamad Bakar Hamad (wakwanza kulia) akisikiliza maelezo kutoka kwa Ofisa wa PURA, Ebeneza Mollel mara baada ya kutembelea banda la Taasisi hiyo wakati wa maonesho ya 49 ya Sabasaba.
Picha: Elizabeth Zaya
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Captain Hamad Bakar Hamad (wakwanza kulia) akisikiliza maelezo kutoka kwa Ofisa wa PURA, Ebeneza Mollel mara baada ya kutembelea banda la Taasisi hiyo wakati wa maonesho ya 49 ya Sabasaba.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Captain Hamad Bakar Hamas, amezipongeza Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) ya Tanzania Bara na Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPRA) kwa kuendeleza mashirikiano ya kisekta.

Ametoa pongezi hizo jana, alipotembelea banda la PURA wakati wa maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam(DITF) yanayoendelea katika viwanja vya Saba Saba Jijini Dar es Salaam.

Akitoa maelezo kwa kiongozi huyo, Mjiolojia mwandamizi kutoka PURA,  Ebeneza Mollel amesema tangu kusainiwa kwa Hati ya Mashirikiano kati ya PURA na ZPRA mwaka 2022, taasisi hizo zimekuwa zikishirikiana kwa karibu katika masuala mbalimbali kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo.

Miongoni mwa maeneo hayo ni pamoja na usimamizi wa data za petroli, ukaguzi wa gharama za uwekezaji na uandaaji wa sheria, kanuni na miongozo mbalimbali.

Maeneo mengine ni udhibiti na usimamizi wa shughuli za mkondo wa juu wa petroli na ushiriki wa wananchi katika shughuli hizo

“Nitumie fursa hii kukujulisha kuwa taasisi hizi zimeendelea kutekeleza Hati ya Mashirikiano na wiki iliyopita, Julai 01, 2025, menejimenti ya PURA na ZPRA zimefanya kikao cha sita kujadili taarifa ya utekelezaji wa Hati ya Mashirikiano kwa mwaka 2024/25” meeleza Ebeneza.

Kufuatia maelezo hayo, Capt. Hamad ametoa pongezi kwa namna ambavyo PURA na ZPRA zimeendelea kushirikiana na kutoa rai kwa taasisi hizo kuyaenzi mashirikiano hayo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Captain Hamad Bakar Hamad akisain katika daftari la wageni mara baada ya kutembelea banda la PURA wakati wa maonesho ya 49 ya Saba Saba yanayoendelea Dar es Salaam.