RC Senyamule: Vijana tumieni ujuzi wa ufundi kufanikisha ndoto zenu

By Ibrahim Joseph , Nipashe
Published at 06:09 PM Jul 08 2025
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ,Rosemary Senyamule
Picha: Ibrahim Joseph
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ,Rosemary Senyamule

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ,Rosemary Senyamule amewataka vijana kutumia fursa ya ujuzi wa mafunzo ya ufundi wanayopata ili kutimiza ndoto zao za maisha.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amewahimiza vijana waliopata mafunzo ya ufundi kutumia ujuzi huo kama nyenzo ya kujiajiri, kutimiza ndoto zao, na kusaidia wengine kupitia fursa walizonazo.

Senyamule alitoa wito huo leo, Julai 8, 2025, jijini Dodoma wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa kwa vijana waliomaliza mafunzo ya ufundi, msaada uliotolewa na Shirika la Tanzania Home Economics Association (TAHEA).

“Serikali haiwezi kuwaajiri watu wote, lakini kupitia ujuzi wa ufundi mlioupata, mnaweza kujiendeleza kimaisha na hata kuwaajiri wengine. Hii ni fursa ya kutimiza ndoto zenu,” alisema Senyamule.

Aidha, aliipongeza TAHEA kwa jitihada zake za kuwawezesha vijana, akisema kuwa mashirika ya kijamii yanayoelekeza nguvu kwa kundi hilo muhimu yanatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake, Meneja Mradi wa TAHEA, Florence Seme, alisema shirika hilo linaendelea kuwajengea uwezo vijana kwa kuwalipia ada za shule za ufundi, kuwapa elimu ya afya ya uzazi, pamoja na kuwawezesha kwa vitendea kazi vya kuanzia maisha.

Alifafanua kuwa katika awamu hiyo, vijana wawili walipewa msaada wa vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni nne kila mmoja. Mmoja alipewa vifaa vyote kwa ajili ya saluni ya wanawake, na mwingine vifaa kamili vya kuanzisha mgahawa. Kila mmoja pia alilipiwa kodi ya miezi mitatu ya eneo la biashara.

“Lengo letu ni kuona vijana hawa wanakuwa na mwanzo mzuri na endelevu wa maisha ya kujitegemea,” alisema Florence.

Shirika la TAHEA limekuwa mstari wa mbele katika kutoa mafunzo ya ujasiriamali, afya ya uzazi, na stadi za maisha kwa vijana katika maeneo mbalimbali nchini.

1