Kiongozi wa zamani wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, ameendelea kuhamasisha Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu ujao, akisisitiza umuhimu wa kuwa na uwakilishi imara bungeni.
Akihutubia wakazi wa Jimbo la Songea, Zitto alisema;
"Lazima tuendelee kupambana. Lazima tuingie kwenye uchaguzi. Lazima tujipange kuhakikisha tunaingiza bungeni wabunge wa kutosha. Ili hoja kama za Buzwagi ziweze kuingia bungeni na kuwanufaisha Watanzania."
Kauli hiyo imekuja wakati ambapo mijadala kuhusu uwajibikaji wa viongozi na usimamizi wa rasilimali za taifa inazidi kushika kasi. Zitto, ambaye alikumbukwa kwa mapambano yake dhidi ya ubadhirifu kwenye sekta ya madini hasa wakati wa mjadala wa mgodi wa Buzwagi mwaka 2007, alisisitiza kuwa mageuzi ya kweli hayawezi kupatikana bila kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kidemokrasia.
Chama cha ACT Wazalendo bado kinaendelea na Operesheni yake waliyoiita Operesheni Majimaji ikiwa na madhumuni ya kuhamasisha watu kushiriki uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED