Fauzia Rajab Shaban, mwanafunzi mwenye ualbino kutoka Kisauni, Zanzibar, aliyehitimu kidato cha sita na kupata ufaulu wa daraja la kwanza, ameeleza kuguswa na kusikitishwa kwake na matukio ya ukatili wa kijinsia pamoja na mauaji ya watu wenye ualbino nchini.
Fauzia, ambaye amemaliza masomo yake katika Shule ya Serikali ya Kiponda mjini Zanzibar, ni miongoni mwa wanafunzi 11,132 waliopata daraja la kwanza katika tahasusi ya HGL (History, Geography, Language), kufuatia kutangazwa kwa matokeo ya kidato cha sita na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) mnamo Julai 7, 2025.
Akizungumza na Nipashe Digital Julai 8,2025 Fauzia amesema kuwa vitendo vya kikatili dhidi ya watu wenye ualbino bado ni changamoto kubwa, hasa vinapochochewa na imani potofu za kishirikina ambazo zinadai kuwa viungo vya watu hao vinaweza kuleta mafanikio au bahati katika maisha ya wengine.
“Wapo watu ambao bado wanaamini kuwa viungo vya watu wenye ulemavu, hasa wenye ualbino, vinaweza kuwa suluhisho la matatizo yao. Vitendo hivi huwa vinashtua sana, hasa kipindi cha uchaguzi mkuu ambapo matukio ya kikatili huongezeka,” amesema Fauzia kwa masikitiko.
Ameongeza kuwa anadhamiria kusoma sheria ili kutetea haki za watu wenye ulemavu na makundi mengine yaliyo pembezoni, huku akieleza pia ndoto yake ya baadaye kuwa mwanasiasa mashuhuri.
“Nataka kuwa mwanasheria kutetea haki za watu kama mimi, lakini pia ndoto yangu ni kuwa Mbunge au Rais wa nchi ili niwe sehemu ya maamuzi makubwa kwa ajili ya haki na usawa,” amesema kwa kujiamini.
Kwa mujibu wa taarifa ya Baraza la Mitihani, mwaka huu ufaulu umeongezeka, ambapo jumla ya 125,779 kati ya 125,847 waliofanya mtihani wamefaulu kwa kupata madaraja ya kwanza hadi la nne, sawa na asilimia 99.95 ya watahiniwa wote.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED