Jokate: Vijana ni nguzo ya ukombozi wa Bara la Afrika

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:15 AM Jul 10 2025
Katibu Mkuu wa UVCCM, Jokate Mwegelo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu Mkuu wa UVCCM, Jokate Mwegelo.

Katibu Mkuu wa UVCCM, Jokate Mwegelo (MNEC) amesema Vijana wa Afrika wasichukuliwe kama watazamaji wa historia bali wawe watekelezaji wakuu wa dira mpya ya ukombozi wa Afrika wa kiuchumi, kidijitali na kisiasa.

Jokate amesema hayo Julai 08 2025 alipowasilisha mada kwenye mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao ambapo Makatibu Wakuu wa Jumuiya za Vijana kutoka nchi za ukombozi ZANU-PF, SWAPO, FRELIMO, MPLA, ANC walishiriki na kiliendeshwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya vijana wa ANC, Cde. Mntuwoxolo Ngudle.

Mkutano huo wa jana ni sehemu ya maandalizi ya mkutano mkubwa utakaofanyika nchini Afrika Kusini mwisho wa mwezi huu.

Katika hotuba yake alieleza kuwa miradi mikubwa ya kimkakati kama Reli ya Kisasa ya SGR inayounganisha Tanzania, Burundi na DRC ni zaidi ya miundombinu, ni alama ya mshikamano wa Afrika na chombo cha ukombozi wa kiuchumi. UVCCM kwa ushirikiano na Serikali ya Rais Dkt. Samia imehakikisha kuwa vijana wanashiriki moja kwa moja katika ujenzi wa miradi hiyo wakijifunza kujiajiri.

Aligusia suala la usimamizi wa rasilimali za Afrika kwa kusema; "Africa's mineral wealth must serve African people first" ambapo aliwataka vijana kutobaki nyuma katika sekta ya madini, bali wawe sehemu ya mabadiliko ya kisera, kimuundo na kimaadili katika uchimbaji na usimamizi wa rasilimali.

Pia aliongelea mapinduzi ya viwanda, alibainisha jinsi ambavyo UVCCM imefanikiwa kushirikiana na mamlaka za mikoa na wilaya kuibua viwanda vidogo na vya kati vinavyoendeshwa na vijana na kuvipa kipaumbele cha kitaifa. 

Alisisitiza suala hilo UVCCM ilikifikisha katika uandaaji wa ilani ya Uchaguzi ya CCM 2025-2030 na hadi kufanikisha kuingizwa ambapo ilani imeeleza; "Kuweka mazingira maalumu ya kuvutia ujenzi wa viwanda vidogo vijijini kwa lengo la kufanya ongezeko la awali la thamani (primary processing) katika sekta za kimkakati zikiwamo kilimo, mifugo, uvuvi, na misitu ili kuongeza fursa za ajira na kupunguza upotevu wa mazao,"

Kuhusu sera na uwezeshaji, Jokate aliipongeza Serikali ya Rais Dk. Samia  kwa kutekeleza sera ya asilimia 10 ya mapato ya halmashauri kutengwa kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu ambapo katika miaka mitano 2020-2025 kiasi cha shilingi bilioni 240.9 zilitolewa kwa mchanganuo ufuatao: shilingi bilioni 96.3 kwa vijana 8,242, shilingi bilioni 45.1 kwa watu wenye ulemavu 1,196, na shilingi bilioni 99.5 kwa Wanawake. 

Aidha, mikopo yenye masharti nafuu ya shilingi 3,197,403,492 ilitolewa kwa vijana kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana akieleza kuwa hatua hiyo imezalisha miradi ya kilimo, biashara, usafirishai na huduma huku ikitoa ajira.

Alihitimisha kwa kuzungumzia dira ya kidijitali ya Afrika, amesema "The internet platforms and data must no longer be foreign-controlled terrain. They Must become Africa's sovereign domain, led by our youth" ambapo kwa Tanzania mpango wa Samia Innovation Fund unalenga kuendeleza vijana wabunifu wa teknolojia ambao ni uelekeo wa dunia ya sasa.