MAMLAKA ya Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), imesema mwamko wa Watanzania kwenye shughuli za mkondo wa juu wa petroli hasa za utafutaji, umeongezeka kwa kiwango kikubwa.
Kauli hiyo imetolewa leo, Julai 09, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Mhandisi Charles Sangweni wakati akizungumza waandishi wa habari ndani ya banda la PURA kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), yanayoendelea kwenye viwanja vya Sabasaba.
Sangweni, amesema wakati shughuli hizo zinaanza, ushiriki wa watanzania hasa kwenye ajira na makampuni ulikuwa chini ya asilimia 55 lakini kwa sasa, umeongezeka hadi kufikia 85.
"Hali hii tunaipima kwa kuangalia makampuni ambayo yamekuwa yakishiriki kwenye shughuli mbalimbali ikiwamo kukusanya data kwa ajili ya kuangalia kama kuna uwezekano wa mahali kunapatikana mafuta, kwenye uchimbaji wenyewe.
" Na tumekuwa na kampeni za hivi karibuni, ya kwanza ambayo ilikuwa kubwa na ya kuonekana ilifanyika bahari kuu mwaka 2018, tulichimba kisima kimoja na timu iliyokuwa kwenye meli ya uchimbaji, kati ya wafanyakazi 150, kwa mara ya kwanza tulikuwa na wafanyakazi 52 wazawa," amesema Sangweni.
Amesema awali walizoea kazi hizo zinafanywa na wageni lakini sasa hivi Watanzania nao ni wengi na idadi yao kubwa wamepata uzoefu kutoka nje ya nchi na wengine uzoefu wao wameupata kutokana miradi mbalimbali ambayo ilifanyika huko nyuma.
"Na sasa hivi tuko kwenye maandalizi ya kuchimba visima vitatu mkoani Mtwara lakini ushiriki wa Watanzania katika mradi huo ni TPDC ambayo inashiriki kwa asilimia 40," amesema.
Sangweni, amesisitiza kwamba, hadi sasa wanahakikisha kwamba kazi ambazo zinaweza kufanyika na makampuni ya Kitanzania zinatekelezwa na makampuni hayo ya kizawa.
Amesema kwa sasa, kila makampuni 10 ambayo wanayaweka kwenye kazi hizo, zaidi ya makampuni sita yanakuwa ya Kitanzania.
"Ni vita lakini tunajitahidi kupigana, ili kuhakikisha Watanzania wanafaidika. Hata hivyo kwenye haya makampuni ambayo yametoka nje, nafasi nyingi ambazo zilikuwa ni za watumishi, hasa za juu za uongozi, zilikuwa zinaenda kwa wenzetu wa nje, lakini leo ukienda kwenye makampuni makubwa, karibu asilimia 95 ya viongozi wa hayo makampuni ni watanzania.
"Hiyo ni faraja kubwa. Kuna maeneo ambayo kama mwenye kampuni au mmiliki hawezi kuyaachia, lakini tunajitahidi kwamba yale maeneo mengine wafanye watanzania," amesema.
Ameipongeza serikali kwa mwamko mkubwa kwenye jambo hilo na kwamba si rahisi kupata hizo nafasi na kuzitumia kama hakuna watu au makampuni yenye uwezo wa kutekeleza hayo majukumu.
"Kwa hiyo kwenye suala la ajira, serikali kama mnafahamu ilifanya juhudi za makusudi kupitia vyuo vikuu, kumekuwa sasa na kozi mbalimbai zinazohusu mafuta na gesi, hivyo wanaohitimu inakuwa ni rahisi kuwatumia kuhakikisha wanapata ajira kama watanzania kwenye haya makampuni.
"Kwa hiyo improvement ni kubwa na ushiriki wetu umekuwa ni mkubwa sana na tunajivunia hilo, tutasimamia lakini unapoona matokeo yanakuwa chanya wewe kama msimamizi lazima ufurahi na kuridhika kwamba kazi yako imefanyika," amesema Sangweni.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED