Upande wa utetezi umepinga Mkemia kutoka Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Edward Dilunga kutoa kielelezo cha dawa za kulevya aina ya heroine kilo 1.02 mahakamani wakidai hana sifa ya kufanya hivyo.
Mapingamizi hayo yaliwasilishwa jana Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi mbele ya Jaji Godfrey Isaya wakati shahidi huyo wa Jamhuri akitoa ushahidi kwa kuongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mafuru Moses.
Washtakiwa katika shauri hilo ni Saidi Rashidi na George David ambao wanashtakiwa kwa kusafirisha kilo 1.02 za heroine, walikamatwa maeneo ya Mivinjeni, Temeke Juni, 2021.
Akitoa ushahidi alidai alipokea sampuli kutoka kwa Selemani Mbwambo, ilikuwa bahasha ya kaki ndani ikiwa na chenga chenga zilizodhaniwa kuwa dawa za kulevya.
Alidai alifanyia uchunguzi sampuli hizo na baada ya uchunguzi alibaini chenga chenga zilikuwa dawa za kulevya aina ya heroine.
Shahidi alikitambua kielelezo na kuomba Mahakama ipokee kama sehemu ya ushahidi wake.
"Naomba Mahakama ipokee dawa za kulevya kama kielelezo nilichokifanyia uchunguzi na kuthibitisha kuwa ni dawa za kulevya aina ya heroine,"alidai shahidi.
Mawakili wa upande wa utetezi walipotakiwa kujibu maombi hayo walipinga.
Wakili Nehemiah Nkoko akiwasilisha pingamizi alidai shahidi hana sifa ya kutoa kielelezo hicho mahakamani .
Alidai Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) katika muongozo wa Jeshi la Polisi (PGO) katoa utaratibu nani anatakiwa kutoa kielelezo mahakamani.
"Ni rai yetu kielelezo kisipokewe, shahidi hana sifa kwani si Afisa wa Polisi aliyekamata,"alidai Nehemiah.
Akijibu Wakili Mafuru alidai hoja za pingamizi za upande wa utetezi hazina mashiko zitupiliwe mbali.
Alidai msimamo sio sahihi kwamba askari aliyekamata ndiye anayestahili kutoa kielelezo mahakamani , aliomba kielelezo kipokewe.
Akiwasilisha hoja Wakili Jeremiah Mtobesya aliomba hoja walizowasilisha upande wa utetezi zionekane zina mashiko, Mahakama ikatae ombi la shahidi kutoa kielelezo cha dawa mahakamani sababu hana sifa.
Jaji Isaya baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili aliahirisha kesi hadi Leo kwa ajili ya kutoa uamuzi wa kupokea au kutopokea kielelezo hicho.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED