Mhitimu kiziwi afaulu bila mkalimani, aomba lugha ya alama iingizwe rasmi mitaala ya elimu

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 06:16 PM Jul 09 2025
Abdul-Azizi Khamis Ali
Picha: Mpigapicha Wetu
Abdul-Azizi Khamis Ali

Abdul-Azizi Khamis Ali, kijana mwenye uziwi aliyehitimu kidato cha sita mwaka huu katika Shule ya Serikali ya Lumumba visiwani Zanzibar, ameibua kilio cha kundi la watu wenye ulemavu wa kusikia kwa kutoa wito wa kuwepo kwa wakalimani wa lugha ya alama katika shule za sekondari na vyuo.

Akizungumza na Nipashe Digital leo Julai 9, Abdul-Azizi ambaye alipata ufaulu wa daraja la pili katika tahasusi ya PCM (Fizikia, Kemia na Hisabati), amesema hakuamini kama angefaulu kwa kiwango hicho kutokana na changamoto kubwa ya kukosekana kwa mkalimani shuleni.

"Nimepambana sana. Hakukuwa na mkalimani hata siku moja darasani wala wakati wa mitihani. Lakini sikukata tamaa. Nimefanya juhudi zangu, nikisaidiwa na walimu, wazazi na marafiki wa karibu,” amesema Abdul-Azizi kwa msaada wa mkalimani wa kujitolea.

Ingawa Serikali ya Zanzibar imepiga hatua katika kuboresha miundombinu ya elimu kwa watu wenye ulemavu, bado amesema suala la lugha ya alama halijawekewa uzito unaostahili katika mfumo rasmi wa elimu nchini.

"Ni muhimu lugha ya alama iwe sehemu ya mtaala kuanzia elimu ya awali hadi elimu ya juu. Viziwi tukipewa wakalimani tunaweza kufanya makubwa. Tuna ndoto kama wengine," ameongeza kwa msisitizo.

Ndoto yake yazimwa na Ukosefu wa Mkalimani

Abdul-Azizi amesema ndoto yake ya kuwa daktari wa binadamu huenda ikayeyuka kutokana na changamoto ya kupata elimu bila msaada wa mtafsiri wa lugha ya alama.

"Nimeamua kusomea utalamu wa vifaa tiba vya afya kwa sababu sina mkalimani na masomo ya vifaa tiba ni nafuu kidogo kulinganisha na udaktari wa binadamu,” amesema kwa masikitiko.

Amekumbuka pia kuwa mwaka 2022, alipata ufaulu wa daraja la pili katika sayansi kwenye mtihani wa kidato cha nne, ambapo alielekezwa kuchukua tahasusi ya PCB (Fizikia, Kemia na Baiolojia), lakini alilazimika kubadilisha na kuchukua PCM kutokana na hali ngumu ya kutokuwa na mkalimani.

Aomba msaada wa kifedha kufikia ndoto zake

Kwa sasa, Abdul-Azizi anaiomba jamii, mashirika ya kijamii, na serikali kumsaidia kifedha ili aweze kujiunga na elimu ya juu na kutimiza ndoto zake za kuchangia taifa kupitia sekta ya afya.

"Naomba msaada wa kifedha ili niweze kuendelea na masomo. Niko tayari kujifunza kwa bidii na kurudisha huduma kwa jamii yangu na taifa," amesema kwa matumaini.

Abdul-Azizi ni miongoni mwa wanafunzi 125,779 waliofaulu mtihani wa kidato cha sita mwaka huu, matokeo yaliyotangazwa rasmi na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) Julai 7, 2025.