DCEA yabaini maiti kutumika kusafirisha dawa za kulevya

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:39 PM Jul 09 2025
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo.
Picha:Mtandao
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imegundua mbinu mpya ya kihalifu ambapo wahalifu hutumia maiti za binadamu kusafirisha dawa za kulevya kutoka nje ya nchi. Dawa hizo hufichwa ndani ya fuvu na kifua cha maiti, kisha miili hiyo kuingizwa nchini kama mizigo ya kawaida.

Akizungumza na wanahabari leo Julai 09,2025 Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema mbinu hiyo imeanza kushindikana kutokana na uwepo wa mitambo ya kisasa ya kuchunguza miili kabla ya kuwasili. Alitoa wito kwa familia kukagua miili ya wapendwa wao kabla ya kusafirishwa ili kuzuia utapeli huo.

Katika hatua nyingine, mfanyabiashara maarufu wa madini anashikiliwa kwa tuhuma za kusambaza biskuti zenye dawa za kulevya aina ya skanka. Mtuhumiwa alikamatwa mkoani Lindi na uchunguzi uliongoza kugunduliwa kwa kiwanda bubu kilichopo Sinza, Dar es Salaam. Biskuti hizo zilisambazwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Mwanza na Mtwara, zikielekezwa zaidi kwa wafanyabiashara wa madini walioko migodini.

DCEA pia iliwakamata raia wawili wa China, Chein Bai na Qixian Xin, wakikutwa na dawa za methamphetamine, ketamine, na vidonge vya frunitrazepam, ambazo ni hatari kiafya na husababisha kupoteza kumbukumbu na kupelekea vitendo vya kihalifu.

Kati ya Mei hadi Julai mwaka huu, DCEA ilikamata dawa za kulevya zenye uzito wa kilo 37,197.142, zikiwemo Mitragyna speciosa (dawa mpya), bangi, heroin, na kemikali bashirifu. Aidha, ekari 1,045.5 za mashamba ya bangi ziliteketezwa katika mikoa mbalimbali.

Kamishna Lyimo ameonya raia wa kigeni na Watanzania wanaoshirikiana nao kwenye biashara hiyo haramu, akisisitiza kuwa sheria za Tanzania hazitambui uraia wala cheo cha mtu anayejihusisha na uhalifu huo.