MWANAFUNZI wa mwaka wa tatu wa Shahada ya Awali ya Sayansi katika Mifumo ya Habari za Afya ( HIS) kutoka Shule Kuu ya Uuguzi na Afya ya Jamii (SoNPH) Lucas Allen Haule(24) ameibuka mshindi wa Kwanza wa bunifu ya Utengenezaji wa Nembo ya Made in Tanzania ambapo lilihusisha zaidi ya washiriki 80 nchini.
Shindano hilo lililaratibiwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), katika Ukumbi wa Karume, Sabasaba, amekabidhiwa zawadi ya Ushindi na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe.
Aidha nembo hiyo ilizunduliwa rasmi Julai 7, 2025 na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, Sabasaba.
Chapa hiyo itawapa wauzaji wa nje jukwaa la pamoja la kupunguza gharama za masoko kwa kuviweka bidhaa chini ya lebo moja inayoaminika.
Lulu amesema jumla ya michoro 88 iliwasilishwa kutoka pande mbalimbali za nchi washiriki 10 bora walichaguliwa na kusaidiwa kitaalamu kuboresha kazi zao kati yao nembo tatu bora ziliingizwa kwenye upigaji kura wa wazi kwa wananchi, nembo ya Haule ilipata kura nyingi zaidi.
Amefafanua nembo hiyo italenga kuleta utambulisho wa pamoja kwa lengo la kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika sekta mbalimbali kama vile kilimo, viwanda, utalii na huduma.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, amesema mpango huo wa chapa ya taifa inalenga kujenga imani kwa walaji na kuongeza mwonekano wa bidhaa za Tanzania.
Akiongea mara baada ya ushindi huo, mwanafunzi Haule amesema aliona tangazo kupitia mtandao wa kijamii Instagram lakini alijisemea hatoweza lakini kuna nguvu ilisema anaweza.
Haule amesema alikuwa akijifunza ubunifu kwa njia ya mtandao kupitia mafunzo ya bure.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED