Kesi ya rufani waliotumwa na afande kuendelea Agosti 5, 2025

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 10:18 AM Jul 10 2025
Kesi ya rufani waliotumwa na afande kuendelea Agosti 5, 2025
Picha: Mtandao
Kesi ya rufani waliotumwa na afande kuendelea Agosti 5, 2025

Kesi ya rufani iliyofunguliwa na washtakiwa wanne waliopatikana na hatia ya kumbaka na kumuingilia kinyume na maumbile binti mkazi wa Yombo aliyetambulisha kwa jina XY, wa mkoani Dar es Saalam itaendelea kusikilizwa Agost 5, 2025.

Kesi hiyo ipo mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma Amir Mruma, ikiwa ni sehemu ya mchakato wa rufaa uliowasilishwa na washtakiwa hao baada ya kutoridhika na hukumu iliyotolewa Septemba 30, 2024, na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, Zabibu Mpangule. 

Washtakiwa hao ni pamoja na askari wa Jeshi la Wannachi wa Tanzania (JWTZ) MT 140105 Clinton Damas (maarufu Nyundo), C.1693 Praygod Mushi, askari wa Jeshi la Magereza, Nickson Jackson (maarufu Machuche), Amin Lema (anayetambulika pia kama Kindamba). 

Wakili wa utetezi, Godfrey Wasonga, akizungumza na waandishi wa habari jana jijini nje ya Mahakama hiyo alidai kuwa baada ya wao kuwasilisha hoja 33 za kutoridhishwa na hukumu iliyotolewa upande wa serikali ulipatiwa muda wa kujibu. 

Alisema baada ya upande wa serikali kujibu hoja hizo Mahakama imeamua kuwapa muda wa kuipitia tena video iliyo rekodiwa na kusambaaa kwenye mitanadao ikionyesha tukio hilo la ubakaji na kuingiliwa kuinyume na maumbile. 

“Mahakama imesema kuwa tutakuja tena Agosti 5, mwaka huu kwa ajili ya shahidi namba moja ambaye ni mtaalamu wa makosa ya mtandaoni ataletwa mbele ya mahakama hii lakini pia imetoa muda kwa mawakili wa serikali kupitia upya video ile. 

“Sisi tumekubali maamuzi ya mahakama na siku zote huwezi kupinga maamuzi ya mahakama iwe umeyapenda ama kuhuyapenda lakini hadi sasa mwenendo wa kesi unakwenda vizuri na maamuzi yote yanatolewa kwa haki,”alisema 

Septemba 30, 2024, Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Dodoma, chini ya Hakimu Mkadhi Mfawidhi Zabibu Mpangule iliwahukumu kifugo cha maisha washitakiwa wote wanne na faini ya Sh. milioni moja kwa kila mmoja wao. 

Kesi hii ya jinai namba 23476 ya mwaka 2024 ilikuwa inawakabili Washtakiwa wanne akiwamo MT 140105 Clinton Damas maarufu Nyundo ambaye ni Askari wa JWTZ, Askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson ‘Machuche’ na Amin Lema anayejulikana pia kwa jina la Kindamba.

Kesi hiyo maarufu ‘Waliotumwa na Afande’ ilisikilizwa faragha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma ambapo upande wa Jamhuri uliwasilisha Mashahidi 18 na vielelezo 12 kuthibitisha mashtaka dhidi ya Washtakiwa.

Washtakiwa hao walifikishwa Mahakamani kwa mara ya kwanza August 19, 2024 na kusomewa mashtaka mawili ya kubaka kwa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile Binti huyo ambaye Mahakamani anatambulika kwa jila la XY ambapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Zabibu Mpangule Washtakiwa hao baada ya kusomewa mashataka walikana na kutokana na unyeti wa kesi hiyo hawakupatiwa dhamana ambapo baada ya kesi kusikilizwa mfululizo walisomewa hukumu na kukutwa na hatia hivyo kuhukumiwa kifungo cha maisha.