Wadau wa mazingira wasafisha ufukwe bahari ya Hindi

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 08:48 PM Jun 16 2025
Wadau wa mazingira wakisafisha fukwe bahari ya Hindi
Picha: Mpigapicha Wetu
Wadau wa mazingira wakisafisha fukwe bahari ya Hindi

TAKRIBANI tani moja za taka, zikiwamo za plastiki zisizooza, zilizokuwa zikitishia afya ya viumbe hai na mifumo ya ikolojia, zimekusanywa kwenye fukwe na bahari ya Hindi.

Mkuu wa Mawasiliano, Masoko na Chapa wa benki hiyo nchini, Desderia Mwegelo, amesema hayo mwishoni mwa wiki Dar es Salaam, akisema huo ni utamaduni wa kila mwaka wa benki hiyo.

“Zaidi ya wafanyakazi 70 wa benki hiyo, wakishirikiana na familia zao, wamefanya usafi katika fukwe za Rungwe jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani.

“Pia kuchangia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hasa namba 13, 14 na 17,” amesema Mwengelo.

Mifuko 100 iliyojaa taka hasa zisizooza ilikusanywa
Ameongeza kwamba usafi hutekelezwa kila mwaka, kwa kushirikiana na shirika la mazingira la Nipe Fagio, huku ikichagua fukwe tofauti kama ishara ya dhamira ya kuhifadhi mazingira ya pwani na kuongeza ushiriki wa jamii.

“Kukusanya karibu mifuko 100 ya taka ni mafanikio, lakini pia ni ukumbusho wa wazi wa hitaji la kuchukua hatua endelevu kwa pamoja,” amesisitiza Mwegelo.

Amesema pia, uhamasishaji wa matumizi ya nishati mbadala katika ofisi husistizwa na programu za kuwajengea wafanyakazi uelewa kuhusu mabadiliko ya tabianchi hutolewa.

“Kwa kushirikiana na mashirika ya kijamii tunaendelea kujizatiti kuwa nguvu chanya katika jamii, kuchangia  maendeleo ya kiuchumi, pia ulinzi wa mazingira kwa vizazi vya sasa na vijavyo.”