Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amewaondoa mawakili wake 30 waliokuwa wakimtetea katika kesi ya uhaini inayomkabili, akieleza kuwa hana muda wa kuzungumza nao akiwa gerezani na hataki wabebeshwe lawama kwa lolote litakalotokea.
Pia amesema wale wanaodhani hatoweza kujiwakilisha wamechemsha kwa sababu ni Wakili wa Mahakama Kuu kwa miaka 22 na amewahi kushughulikia kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Lissu ametoa kauli hiyo leo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Franco Kiswaga, akieleza pia changamoto anazopitia akiwa gerezani, ikiwemo kufungwa sehemu moja na watu waliokwishahukumiwa kunyongwa na kulindwa na askari wawili kila anapokwenda.
Amesema kwa siku 68 alizokaa mahabusu imeshindikana kuzungumza na mawakili wake na akaona isiwe sababu ya wao kulaumiwa na kuonekana hawajamtetea ipasavyo.
“Sitaki hata wakili mmoja alaumiwe kwa kosa ambalo si lake, na kwa sababu hiyo nakupa taarifa kwamba kuanzia leo nitajitetea mwenyewe,” amesema Lissu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED