Mamlaka ya Usafiri wa Ardhini (LATRA) imezitaka kampuni zinazotoa huduma ya tiketi mtandao kwa mabasi kuhakikisha zinaunganisha mifumo yao na mfumo wa serikali pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hadi kufikia Juni 30, vinginevyo zitachukuliwa hatua kali.
Onyo hilo limetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa LATRA, Salum Pazzy, wakati wa ukaguzi wa kushtukiza katika Stendi Kuu ya mabasi yaendayo mikoani ya Msamvu iliyopo Manispaa ya Morogoro.
Alisema LATRA itaendelea kutoa huduma kwa kampuni ambazo zimeidhinishwa na serikali na si vinginevyo.
“Ifikapo Julai Mosi mwaka huu, watoa huduma wa mifumo ya tiketi mtandao ambao hawajaunganisha mifumo yao na mfumo wa serikali hawatoruhusiwa kuendelea kutoa huduma. LATRA tutaendelea kutoa huduma kwa wale waliojiunganisha tu na mfumo wa serikali,” alisema Pazzy.
Aidha, alisema ifikapo Julai Mosi mwaka huu, LATRA itawatangazia wananchi watoa huduma wa mfumo wa tiketi mtandao waliokamilisha taratibu za mifumo hiyo kusomana na ule wa serikali.
Kuhusu ukaguzi, Pazzy alisema ulihusisha kuangalia uwekaji wa alama kwenye mizigo ya abiria, matumizi ya mikanda ya usalama, na matumizi ya tiketi mtandao ambapo wamebaini wasafirishaji wengi wanafuata sheria.
“Tumeona kuna changamoto ambazo zilizokuwepo awali kama matumizi ya tiketi mtandao na mabasi kuwa na mikanda ya usalama, lakini baada ya kuwapa elimu na kuwakumbusha mara kwa mara hivi sasa zimeanza kupungua, na wale wanaofanya uzembe wanapewa adhabu,” alisema Pazzy.
Alisema ukaguzi mwingine ni pamoja na wahudumu wanaotoa huduma kwenye mabasi ambao wanapaswa kuwa wamehudhuria mafunzo yanayotolewa na vyuo mbalimbali vilivyoidhinishwa, na baada ya mafunzo hayo watasajiliwa na LATRA kupitia mfumo kwa ajili ya kukidhi vigezo vya kutoa huduma hizo.
“Tulishatoa maelekezo muda mrefu kuwa watoa huduma wote kwenye mabasi wanapaswa kupata mafunzo kwenye vyuo mbalimbali nchini, na muda umeshakwisha. Hivyo wale ambao hawajasajiliwa LATRA wanapobainika wanapewa adhabu,” alisema Pazzy.
Kuhusu mabadiliko ya sheria yaliyofanyika hivi karibuni na kupitishwa na Bunge, alisema kabla ya mabadiliko hayo jukumu la ukaguzi wa magari kabla ya kuyapa leseni lilikuwa kwenye sheria ya LATRA na Sheria ya Usalama Barabarani, jambo lililosababisha mwingiliano wa majukumu. Baada ya mabadiliko yaliyofanyika, jukumu hilo limeondolewa LATRA na kubaki kwa Jeshi la Polisi.
Mmoja wa wanaotoa huduma katika basi la Kampuni ya Abood linalofanya safari kati ya Dar es Salaam na Bukoba, Stella Joseph, amesema ukaguzi huo wa mara kwa mara unawasaidia kuwakumbusha watoa huduma kutimiza wajibu wao na kufuata taratibu mbalimbali.
“Wapo wahudumu wengine kwenye mabasi utakuta wanafungulia muziki au TV kwa sauti kubwa na kuleta bughudha kwa abiria, kitu ambacho kama umepitia mafunzo huwezi kukifanya. Hivyo ni vyema ukaguzi huu ukafanyika mara kwa mara,” alisema Stella.
Naye Jackline Fadhili, mhudumu wa basi la Kampuni ya Saratoga linalofanya safari kati ya Kigoma na Dar es Salaam, amesema kutokana na LATRA kuweka sheria kali, sasa wanalazimika kufuata maagizo hayo kwa kuwa abiria wengi hivi sasa wameshajua haki zao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED