Akiwa ameendelea kuzuiliwa gerezani kwa zaidi ya siku 200, na zikiwa zimesalia takribani siku 21 kabla ya mwaka kuisha, huenda Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, akalazimika kusherehekea Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya akiwa bado gerezani.
Kesi yake, ambayo kwa mara ya mwisho iliahirishwa Novemba 12 mwaka huu, hadi sasa haijapangiwa tarehe nyingine ya kusikilizwa, huku mwaka wa mahakama ukielekea ukingoni. Kwa mujibu wa Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Rugemeleza Nshala, mwaka wa mahakama unatarajiwa kufungwa Desemba 15, jambo linalopunguza uwezekano wa kesi hiyo kupewa tarehe mpya kabla ya mwaka kuisha.
Lissu alikamatwa kwa mara ya kwanza wilayani Mbinga mkoani Ruvuma wakati akiendelea na ziara ya chama chake. Baadaye alisafirishwa hadi Dar es Salaam ambako alifunguliwa shtaka la uhaini, shtaka ambalo kisheria halina dhamana, na hivyo kumlazimu kuendelea kusalia gerezani tangu wakati huo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED